Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Mikataba ya Geneva juu ya Hifadhi ya maisha na hishima ya wanadamu wasioshiriki kwenye mapigano - hususan, raia, wafanyakazi wa afya, wahudumia misaada ya kiutu, pamoja na wagonjwa, wanajeshi majeruhi na mateka wa vita - imetimia miaka 60 mnamo tarehe ya leo, 12 Agosti 2009. KM ameeleza kwenye taarifa aliotoa juu ya kumbukumbu hiyo kwamba kanuni ya Mikataba ya Geneva zimefanikiwa "kudumishwa na kuvumiliwa na umma wa ulimwengu kwa muda mrefu" kwa sababu ya umuhimu unaopewa sheria hizo na jumuiya ya kimataifa. KM alipendekeza kwa Mataifa Wanachama yote kuchukua hatua zinazofaa, kuhakikisha kanuni za kimsingi za Mikataba ya Geneva huwa zinatekelezwa na wote kama ipasavyo.

Mamia ya wajumbe waliokusanyika mjini Bonn, Ujerumani wiki hii kuhudhuria vikao vya kujadilia mawazo mapya, ya kuharakisha maafikiano ya udhibiti bora wa mabadiliko ya hali ya hewa, kabla ya Mkutano Mkuu ujao utakaofanyika Copenhagen, Denmark mwezi Disemba, leo wameingia siku ya tatu ya mijadala. Yvo de Boer, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya UM kuhusu Mkataba wa Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC) amenakiliwa akisema majadiliano yao sasa hivi yamefikia mwanzo mzuri, kwenye jitihada za serikali wanachama za kupunguza vifungu vya kujadiliwa, kutoka waraka wenye kurasa 200. Alisema maafikiano ya kutia moyo yalishapatikana katika baadhi ya mada, hususan kwenye masuala yanayohusu kusaidia nchi zinazoendelea kupata fedha na teknolojia ya kisasa, ya kutumiwa kupunguza umwagaji wa hewa chafu angani. De Boer alisema mashauriano ya kiufundi mkutanoni, hivi sasa yameunganishwa na makubaliano ya kisiasa yaliopokewa kutoka Mkutano Mkuu wa Mataifa Wanachama wa G-8, pamoja na Mkutano Mkuu juu ya Uchumi uliofanyika mwezi uliopita, mazingira ambayo yamewasilisha matokeo yenye nguvu, na yanayoweza kutendeka kihakika kwenye Mkutano wa Disemba utakaofanyika Copenhagen.

Shirika la UM Linalofarajia Wahamiaji wa KiFalastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA), limetangaza taarifa yenye kuelezea kuwa na wasiwasi juu ya mwelekeo wa karibuni, kuhusu ripoti zisio msingi, zinazotolewa mara kwa mara na vyombo vya habari vya Israel juu ya kazi za UNRWA. Ripoti ya UNRWA ilitoa mfano wa taarifa moja ya karibuni ambayo ilidai ofisa, asiye jina, wa Vikosi vya Ulinzi vya Israel ati alithibitisha kundi la WaFalasatina la Hamas liliteka nyara, kwa kushikia bunduki, magari matatu ya wagonjwa ya UNRWA. UM umekana madai haya na imesisitiza kuwa taarifa hizo hazina msingi, na hata kutoa picha zenye kuonyesha dhahiri magari hayo ya wagonjwa yameegeshwa sasa hivi kwenye uwanja wa majengo ya Makao Makuu ya UNRWA katika Ghaza, na UNRWA ipo tayari kuyapeleka magari hayo kwenye vituo vya ukaguzi vya Israel kuthibitisha wanayoyasema. UNRWA imeshatuma malalamiko yake kwa wenye madaraka Israel, kuhusu ripoti zao zisio sahihi, zinazotolewa mara kwa mara kwenye vyombo vya vya habari vya Israel. UNRWA ilitumai maofisa wa Israel wasio na majina, wanaonakiliwa na vyombo vyao vya habari juu ya taasisi ya UM iliopo Ghaza, watakitahidi kutoa taarifa zenye ukweli, na zilizo sahihi, na sio uvumi usio msingi. Taasisi ya UNRWA ilikumbusha juu ya majukumu yake muhimu ya kuhudumia misaada ya kiutu umma wa eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza, na taarifa za uwongo juu ya shughuli za UNRWA zimegundulikana kuwachanganyishia umma, kwa makusudi, na kuwakosesha kujua ukweli wa hali mbaya ya kiutu inayowakabili WaFalastina milioni 1.5 ambao kwa sasa wanaishi kwenye mazingira yasiostahamilika wala kukubalika kibinadamu. UNRWA imekumbusha tena mwito uliotolewa na Wapatanishi wa Pande Nne juu ya mzozo wa Mashariki ya Kati, uliohimiza vivuko vyote vya ukaguzi vya Ghaza vifunguliwe na kuruhusu kuingizwa Ghaza vifaa vinavyohitajika kujenga tena nyumba 50,000 ziada za WaFalsatina, zilizoangamizwa na kuharibiwa wakati wa mashambulio ya vikosi vya Israel, yaliotukia mwanzo wa mwaka, mashambulio ambayo yaliopewa jina la "Operesheni ya Kumimina Risasi".