Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO itaanza kuripoti maambukizi ya A/H1N1 kila Ijumanne

WHO itaanza kuripoti maambukizi ya A/H1N1 kila Ijumanne

Shirika la Afya Duniani (WHO) limearifu hii leo kutoka mjini Geneva, kwa kupitia msemaji wake Fadéla Chaib, ya kuwa kila Ijumanne litakuwa likitangaza taarifa mpya juu ya maambukizi ya homa ya mafua ya A/H1N1 ulimwenguni.

Ripoti ya leo sasa imebainisha kwamba kuanzia tarehe 06 Agosti 2009, watu 177,457 waliambukizwa na homa ya mafua ya H1N1 katika nchi na maeneo 170 duniani. Kati ya idadi hiyo wagonjwa 1,462 walifariki kutokana na maradhi. Hata hivyo, taarifa ya WHO ilihadharisha kwamba jumla hiyo si kamilifu, kwa sababu mataifa mengi haytarajiwi tena kuchunguza maradhi ya homa kama yanawiana na homa ya mafua ya H1N1. Kadhalika, WHO imetangaza majina ya mataifa yalioripoti maambukizo ya homa ya mafaua ya H1N1, kwa mara ya kwanza - ikijumlisha Azerbaijan, Gabon, Kazakhstan, Jamhuri ya Moldova na Swaziland.