Skip to main content

KM alaumu kifungo ziada cha Aung San Suu Kyi kutoka mahakama ya Myanmar

KM alaumu kifungo ziada cha Aung San Suu Kyi kutoka mahakama ya Myanmar

KM Ban Ki-moon amelaumu uamuzi wa mahakama ya Myanmar, wa kutoa adhabu ziada ya kifungo cha nyumbani cha miezi 18, kwa kiongozi mpinzani na mpokezi wa Tunzo ya Amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi.

KM amewasihi wenye madaraka Myanmar kumwachia "haraka na bila shuruti" Daw Aung San Suu Kyii, na kuwahimiza kufanyisha mazungumzo ya pamoja ili kusuluhisha matatizo yaliolikabili taifa. Taarifa ya KM ilisisitiza ya kuwa "bila ya Aung San Suu Kyi kuachiwa, pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa waliopo kizuizini katika Myanmar, na bila ya kuwaruhusu raia hawa kushiriki kwenye uchaguzi ulio huru na wa haki, imani ya mfumo wa kisiasa nchini humo itatafsiriwa na jumuiya ya kimataifa kuwa mfumo wa wasiwasi na mashaka makubwa." Aung San Suu Kyi anaongoza chama cha upinzani cha Umoja wa Taifa kwa Demokrasia (NLD), na alishtakiwa kukiuka sheria ya usalama wa taifa baada ya raia mmoja wa Marekani alipojiingiza, bila kualikwa, kwenye nyumba ya Aung San Suu Kyi wakati alipokuwa kwenye kizuizi cha nyumbani. Mwanasiasa huyo wa Myanmar ameshatumia miaka 12 ziada chini ya kifungo cha nyumbani.