Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali Usomali yaendelea kuharibika, inahadharisha OCHA

Hali Usomali yaendelea kuharibika, inahadharisha OCHA

Ofisi ya UM juu ya Huduma za Dharura (OCHA) imeripoti, Ijumanne, kutoka Geneva, kwamba hali ya usalama nchini Usomali, kwa ujumla, inaendelea kuharibika wakati mahitaji ya kunusuru maisha yakizidi.

OCHA inasisitiza hali hii hukwamisha zile huduma za kupeleka misaada inayohitajika kunusuru maisha ya umma muhitaji, hasa katika kipindi ambapo fungu hilo hutegemea kufadhiliwa misaada ziada kutoka wahisani wa kimataifa. Takwimu za UM zimeyakinisha kwamba taifa la Usomali ndio lenye kuongoza ulimwenguni kuhusu jumla ya mashambulio dhidi ya wafanyakazi wanaohudumia misaada ya kiutu. Kwa mujibu wa ripoti hizo, katika 2009 wasaidizi wa huduma za kiutu 8 walishauawa Usomali, na tangu 2008 wahudumia misaada ya kihali 19 walishikwa na kuwekwa vizuizini na makundi yasiotambulikana. Kadhalika, Ofisi ya OCHA ilibainisha ya kuwa baina ya miezi ya Mei hadi Julai mwaka huu, maeneo matatu, ambapo majengo ya UM yalipo, katika sehemu za Kusini na Kati nchini Usomali, yalishambuliwa na majeshi ya mgambo. Ripoti ya OCHA imetahadharisha pia kwamba uharamia wa baharini, unaofanyika katika mwambao wa Usomali, nalo ni tatizo kubwa lenye kuzorotisha huduma za misaada inayotakiwa kidharura kukidhi mahitaji ya umma wenye shida nchini humo.