Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Kumbukumbu ya Wahudumia Misaada ya Kiutu Duniani

Siku ya Kumbukumbu ya Wahudumia Misaada ya Kiutu Duniani

Mnamo tarehe 19 Agosti (2009), UM utaadhimisha, kwa mara ya kwanza ‘Siku ya Kumbukumbu ya Wahudumia Misaada ya Kiutu Duniani.\'

' Siku hii ilipitishwa na Baraza Kuu la UM kwa madhumuni ya kuhishimu mchango wa wafanyakazi wote wa mashirika ya kimataifa, waliopoteza maisha wakati wakihudumia misaada ya kiutu kwa jamii zenye dhiki na shida katika sehemu mbalimbali za dunia. Miongoni mwao alijumuika mtaalamu maarufu, aliyejitolea mhanga kuhudumia umma wenye shida, Sergio Vieira de Mello, ambaye mnamo tarehe 19 Agosti 2003 aliuawa pamoja na wafanyakazi wenzi 21 kwenye shambulio la bomu liliotupwa katika makao makuu ya UM yaliokuwa katika Hoteli ya Canal kwenye mji wa Baghdad, Iraq. Kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA), katika kipindi cha miaka 10, wahudumia misaada ya kiutu 700 walipoteza maisha kutokana na mashambulio dhidi yao, na kwa kutekwa nyara, pamoja na wizi wa kuvamia, kunajisiwa kimabavu na hali nyengine za jinai. OCHA ilisema katika kipindi cha sasa mashambulio dhidi ya wahudumia misaada ya kiutu yamezidi ulimwenguni, hali ambayo huathiri zaidi umma dhaifu unaohitajia misaada ya kunusuru maisha kutoka kwa wafanyakazi hawa wa kimataifa. Takwimu za UM zimethibitisha, katika 2008 jumla ya wahudumia misaada ya kiutu 260 ama waliuawa, au kutekwa nyara na kujeruhiwa vibaya kwenye mashambulio ya kutumia nguvu - na kati ya idadi hiyo wahudumia misaada ya kiutu 122 waliuawa na 62 walitekwa nyara.