Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la UM Kusimamia Ulinzi Amani Sudan Kusini (UNMIS) limeripoti kuwa limefanikiwa kukamilisha awamu ya kwanza ya mradi wa kuwapokonya silaha wapiganaji wa zamani katika Jimbo la Blue Nile, liliopo Sudan kusini. Ijumatatu, kwenye mji wa Ed Damazin wapiganaji wa zamani 5,674 walisalimisha silaha kwa UM. Thuluthi moja ya wapiganaji hawa wameshakamilisha mafunzo juu ya nidhamu zinazotakikana kuwaunganisha tena na maisha ya kikawaida kwenye jamii zao ziliopo katika maeneo ya Jimbo la Nile (Nile State), Kordofan Kusini (Southern Kordofan) na katika Abyei. Mapatano ya Jumla ya Amani ya 2005, baina ya Kaskazini na Sudan Kusini yameamuru wapiganaji wa zamani 180,000 kutoka Jeshi la Sudan, majeshi ya mgambo ya PDF na SPLA kusalimisha silaha zao kwa taasisi za kimataifa kama UNMIS. Mradi huu sasa unakabiliwa na matatizo ya fedha zinazotakikana kuutekeleza kama ilivyodhaminiwa na mapatano ya makundi husika. Mkutano wa kimataifa kuchangisha msaada huo, uliofanyika mwezi Februari kwenye mji wa Juba ulikadiria kwamba wahisani wa kimataifa watahitajia kuchangisha msaada wa fedha wa dola milioni 430 kugharamia kikamilifu mradi wa kupokonya silaha wapiganaji wa zamani, na jumla iliokusanywa kwa sasa kutoka wafadhili wa kimataifa ni dola milioni 88.3 tu.

OCHA imeripoti ya kuwa mchanganyiko wa mapigano makali baina ya vikosi vya serikali na wapinzani, pamoja na ukame unaoenea kwa kasi Usomali, na mizozo ya kiuchumi iliokabili nchi ni mchanganyiko wa matatizo yaliosababisha nusu ya idadi ya raia - yaani Wasomali milioni 3.2 - kutegemea misaada ya kihali kutoka mashirika ya kimataifa kunusuru maisha. Ripoti ya OCHA ilisema udhalilishaji wa raia umekithiri kwenye mazingira haya, mathalan, ajira ya mabavu ya watoto wapiganaji, vitendo vya kutumia nguvu kunajisi raia, na watu kukamatwa kihorera na kuwekwa vizuizini bila ya kufikishwa mahakamani, na pia vitisho, bughudhi na wizi wa mali za watu, mambo ambayo yamethibitisha dhahiri kwamba hali ya usalama nchini inahitajia kudhibitiwa haraka, kwa masilahi ya umma na utulivu wa eneo zima la katika Pembe ya Afrika. Kadhalika, OCHA inasema mzoroto wa uchumi uliopo kwenye soko la kimataifa ni miongoni mwa vigezo vinavyochangisha upaliliaji wa mizozo ya kiutu katika Usomali. Kwa mfano, ripoti iliongeza, mnamo nusu ya mwanzo ya 2009, malipo ya fedha zinazoingia nchini kutoka Wasomali waliotawanyika nchi za nje uliteremka kwa asilimia 25 kwa sababu ya upungufu wa ajira. Lakini juu ya kuwepo mazingira haya hatari na ya kigeugeu, yanayochelewesha operesheni za huduma za dharura Usomali kwa umma muhitaji, wafanyakazi wa mashirika yanayosimamia misaada ya kiutu bado wanaendeleza kazi zao na kugawa vyakula na mahitaji mengine ya kimsingi kwa raia wa Usomali. Hivi sasa UM unahudumia chakula raia milioni 2.2 wa Usomali, kila mwezi; na kila siku huwapatia wahamiaji waliong'olewa makazi 600,000 maji safi na salama, na kuhudumia afya watoto milioni 1.5 pamoja na wanawake milioni moja.
Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limeripoti kuwa litaanzisha upelelezi juu ya shambulio la mkandarasi raia wa Sudan ambaye Ijumatatu alipigwa risasi na kuuawa karibu na kambi ya UNAMID ya El Daein, Sudan Kusini. Wakati huo huo UNAMID imetangaza kuwasili Nyala, Darfur Kusini kwa walinzi amani 133 kutoka Burkina Faso. Askari hawa waliowasili wiki hii kutoka Burkina Faso hujumuisha wahandisi wa kijeshi watakaosaidia kujenga kambi kubwa katika eneo la Foro Baranga, itakayotumiwa na wanajeshi ziada wa kutoka Burkina Faso ambao wanatazamiwa kuwasili katika siku zijazo.

Shirika la Ulinzi Amani la UM katika JKK (MONUC) limehitimisha warsha maalumu wa mafunzo ya kuimarisha kazi za polisi kwa maofisa wa polisi wa Kongo 293, kutoka jimbo la Kasai Magharibi. Mafunzo haya yaliandaliwa bia na Polisi wa Taifa, na yanatarajiwa kuimarisha zaidi utendaji wa kazi za polisi ili kudhibiti vyema utulivu wa jamii. Vile vile mafunzo yamekusudiwa kuhakikisha sheria na kanuni za nchi zitatekelezwana kuhishimiwa wakati wa uchaguzi unaotazamiwa kufanyika katika robo ya mwanzo ya 2010.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti jumla ya raia wa JKK waliong'olewa makazi kwa sababu ya mapigano yalioshtadi karibuni katika Jimbo la Orientale, imekiuka watu 50,000. Kadhalika watu 21,000 ziada wameripotiwa kuelekea Sudan Kusini kuomba hifadhi. WHO inasema inajitahidi kuwapatia wahamiaji wote hawa huduma za afya ya msingi. Hata hivyo, ukosefu wa hali ya usalama inakwamisha shughuli za kukidhi mahitaji ya afya ya wahamiaji hawo, hasa katika Jimbo la Orientale. WHO inakhofua afya ya jamii huenda ikaathirika sana pindi maradhi hatari ya kijamii hayajadhibitiwa mapema, mathalan, malaria, matatizo ya kupumua na huduma za uzazi. Kadhalika kuna hatari ya watoto wadogo kupatwa na maradhi ya utotoni pindi watakosa kuchanjwa mapema, ilihadharisha WHO.

Kwenye mahojiano aliofanya na Redio Okapi, katika JKK, ambayo hushirikiana na UM, Waziri wa Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton alisema taifa lake lipo tayari kujumuika na UM kukomesha vile vitendo karaha vya kutumia mabavu ya kunajisi wanawake kama ndio silaha ya vita, vinavyoendelezwa na wapiganaji waasi, na hata baadhi yawanajeshi wa Serikali, katika eneo la mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Alisema tabia mbaya ya udhalilishaji wa kijinsiya na matumizi ya mabavu dhidi ya wanawake kuwa ndio silaha ya kutishia raia na kuwakatisha tamaa ya kimaisha, kwa makusudio ya kuwalazimisha kuhajiri makwao, vitendo hivi alisisitiza ni lazima vikomeshwe halan nchini humo. Aliahidi kwamba "Marekani, na nchi nyengine wanachama, pamoja na UM yenyewe, wapo tayari kuisaidia Serikali ya JKK kuchukua hatua hakika za kuendeleza mbele haki za binadamu na kuadhibu wale wanaokiuka haki hizo pamoja na wale wanaoharamisha haki za wanawake". Lakini kuweza kuyakamilisha mapendekezo hayo kwa mafanikio, alitilia mkazo, Serikali ya JKK itajitaji kukuza mchango wake kwa ushirikiano na jumuiya ya kimataifa.