Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya kudhibiti marekebisho ya hali ya hewa yameanzisha duru nyengine Bonn

Mazungumzo ya kudhibiti marekebisho ya hali ya hewa yameanzisha duru nyengine Bonn

Hii leo kwenye mji wa Bonn, Ujerumani wajumbe wa kimataifa wamekusanyika tena kwenye duru nyengine ya kikao kisio rasmi, kushauriana juu ya maafikiano yanayotakikana kukamilishwa kwenye Mkutano Mkuu ujao, wa kupunguza umwagaji wa hewa chafu ulimwenguni, utakaofanyika mwezi Disemba mjini Copenhagen, Dennmark.

Kwenye kikao cha Bonn, kilichoanza wiki hii, na kutarajiwa kuchukua siku tano, wawakilishi wa kimataifa 2,000 wanajaribu kusuluhisha kwa makubaliano waraka wa kuzingatiwa kwenye kikao cha Copenhagen. Yvo de Boer, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya UM Inayosimamia Mkataba wa Udhibiti wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC) kwenye risala yake ya ufunguzi alikumbusha kwamba "muda hatunao tena", kwa sababu masuala mengi sana bado yamesalia kwenye waraka, yanayohitaji kurekibishwa haraka kabla ya mwezi Disemba.