Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku Kuu ya Kimataifa kwa Wenyeji wa Asili

Siku Kuu ya Kimataifa kwa Wenyeji wa Asili

Ijumapili, tarehe 09 Agosti, ni siku inayoadhimishwa na jamii ya UM kila mwaka kuwa ni ‘Siku Kuu ya Kimataifa kwa Wenyeji wa Asili Duniani\'.

 Mada ya mwaka huu imekusudia kuwakumbusha walimwengu matatizo yanayowakabili wenyeji wa asili, fungu la umma wa kimataifa unaoshuhudia kiwango cha chini kabisa cha huduma za afya ya msingi, kwa sababu ya kupigwa na ufukara, utapiamlo, uharibifu wa mazingira na huduma nyenginezo zenye kudidimiza zaidi maisha yao duni. Kwenye risala aliotoa KM Ban Ki-moon kuihishimu siku hiyo alizisihi serikali wanachama na jumuiya za kiraia, kwa ujumla, kutenda kidharura, na kwa bidii zaidi, huduma za maendeleo, kwa kushirikiana kikamilifu na wenyeji wa asili ili kuwasaidia kuziba pengo, lilioselelea, la umaskini kwenye jumuiya zao, hususan kwenye sekta ya afya na ilimu. KM alitilia mkazo, kwenye risala yake, umuhimu wa kulenga huduma za maendeleo kwenye sekta ya afya, shughuli zitakazowawezesha wenyeji wa asili kuwa na uwezo wa kupatiwa taarifa kinga ili kugundua mapema maradhi, hasa yale maradhi yanayoambatana na maambukizi ya VVU, hali ambayo baadaye itawawezesha kuyadhibiti maradhi haya maututi yanayohatarisha zaidi jamii zao. Jumla ya wenyeji wa asili, wanaokutikana katika nchi 70 za ulimwengu, imekadiriwa na UM kufikia milioni 370; na ni umma ambao huishi katika sehemu zenye anuwai kubwa ya viumbe hai Duniani, na asilimia kubwa yao, alisema KM, ndio yenye kuzungumza takriban lugha zote za ulimwengu.