Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon sasa hivi anazuru Jamhuri ya Korea (Korea ya Kusini). Ijumatatu, wakati alipokuwa kwenye mji wa Seoul alihutubia Shirikisho la Jumuiya za UM Duniani ambapo alikumbusha walimwengu tunaishi hivi sasa katika umri ulioghumiwa na mizozo ya sehemu nyingi, hali ambayo haiwezi kusuluhishwa na taifa moja pekee. Alitahadharisha ya kuwa si sawa kwa mataifa kudhania mchango wa kuzisaidia nchi maskini kukamilisha Malengo ya Manedeleo ya Milenia ni "sadaka". Alisisitiza mchango huo huwakilisha "mshikamano wa umma wa ulimwengu uliofungamana" na humaanisha maslahi ya binafsi yenye kuthibitisha wanadamu wote wamejumuika kwenye mkondo mmoja wa kimaisha. Aliendelea kwa kuutafsiri mzozo wa Darfur kuwa ni funzo kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu mafanikio na kasoro iliopo kwenye utekelezaji wa ushirikiano mpya wa pande nyingi. Alisisitiza kwamba UM unapopewa majukumu na Baraza la Usalama, hujitahidi kuyatekeleza kwa kadri ya uwezo unaofadhiliwa nawo. Alisema majukumu hayotoweza kukamilishwa kwa mafanikio ikiwa Mataifa Wanachama yanashindwa kutekeleza ahadi zao na kuinyimwa UM vifaa, zana na fedha zinazohitajika kuhudumia, kwa ukamilifu, opersheni inazodhaminiwa nazo kuimarisha uslama na amani kwenye maeneo ya mizozo.

KM Ban Ki-moon ameripotiwa kuyakarbisha maafikiano ya kugawana madaraka baina ya makundi yaliokuwa yakihasimiana mnamo siku za nyuma nchini Bukini. Aliyataka makundi husika yashirikiane kipamoja na kuhakikisha kutabuniwa serikali mpya ya muungano itakayowasilisha mfumo unaoaminika, utakaotumiwa kutayarisha uchaguzi wa taifa katika kipindi kisiokiuka miezi 15 ijayo. Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na msemaji wa KM, Ban Ki-moon aliwapongeza viongozi wanne wa Bukini kwa kuahidi kushirikiana kufanya mageuzi ya amani nchini mwao, kwa kupitia serikali ya muungano wa muda. Viongozi hawo ni Andry Rajoelina, Marc Ravalomanana, Didier Ratsiraka na Albert Zafy. Taarifa ya KM inafuatia muafaka wa Ijumapili uliokubaliwa kwenye mji wa Maputo, Msumbiji baada ya kumalizika majadiliano yaliosimamiwa na raisi wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chissano pamoja na wawakilishi wa kutoka UM, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Afrika (SADC) pamoja na Shirika la Kimataifa kwa Wanaozungumza Kifaransa (Francophonie).

Rodolphe Adada, Mjumbe Maalumu wa Pamoja wa UM-UA kwa Darfur (UNAMID) alikutana mwisho wa wiki iliopita, kwenye mji wa Addis Ababa, na Mwenyekiti wa Tume ya Hadhi ya Juu ya Umoja wa Afrika juu ya Darfur, raisi wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki ambaye alijadilia naye maendeleo yaliojiri karibuni kwenye eneo la Darfur, ikijumlisha suala linalohusu namna mpango wa amani unavyotekelezwa. Mnamo mwezi Septemba Tume ya UA kwa Darfur inatarajiwa kuwakilisha ripoti yake ya mwisho juu ya eneo la mzozo, kufuatia ziara ya karibuni ya uchunguzi iliofanywa na wajumbe wa tume.

Kadhalika, Shirika la Operesheni za Mchanganyiko za UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limetangaza mnamo mwisho wa wiki iliopita, kuwasili Darfur kwa maofisa wa polisi 38 ziada kutoka Uganda ambao walijumlisha nguvu ya polisi wa UNAMID sawa na askari 2140, asilimia 50 ya jumla inayotakikana kuongoza operesheni za mapolisi kwenye jimbo hili la Sudan magharibi.

Young-jin Choi, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Cote d'Ivoire na Mkuu wa Shirika linalosimamia Operesheni za Kulinda Amani katika Cote d'Ivoire (UNOCI) aliwaambia wajumbe waliohudhuria kikao cha saba, cha mfuatilio, cha kamati ya amani ya Cote d'Ivoire, kwenye mji wa Ougadougou, ya kwamba anabashiria mwezi Septemba utawasilisha kipindi muhimu juu ya maamuzi ya uchaguzi nchini humo. Alitarajia orodha ya wapiga kura itakuwa imeshakamilishwa wakati huo, ili kuwawezesha wasimamia uchaguzi kutathminia kikamilifu uchaguzi wa raisi unaotazamiwa kufanyika mwezi Novemba, na vile vile kutathminia jitihadi za kuunganisha taifa. Choi aliyasihi makundi yote ya kisiasa nchini kuhishimu taratibu za uchaguzi, hasa ilivyokuwa wapiga kura milioni 6.5 wamekadiriwa wameshajiandikisha kushiriki kwenye uchaguzi ujao.

Shirika la Usaidizi Amani la UM katika Afghanistan (UNAMA) na Kamisheni Huru ya Haki za Binadamu katika Afghanistan (AIHRC) wamechapisha ripoti ya pamoja yenye kuonyesha hali isiyo ya usalama iliotandaa kwa sasa nchini Afghanistan huathiri sana maandalizi ya uchaguizi ujao, hususan katika ulinzi wa wapiga kura wanawake. Ripoti ilisema licha ya kutangazwa vitisho, ikichanganyika na mashambulio ya hapa na pale, WaAfghani bado wanaendelea kuonyesha hamu kuu ya kutaka kushiriki kwenye upigaji kura wa taifa. Hata hivyo, hali ya wasiwasi hairuhusu raia kuwa na uhuru wa kutembea, na inawafunga kutekeleza haki yao halali ya uhuru wa kusema, hasa wagombea uchaguzi pamoja na wafuasi wao, na kuwazuia kuendeleza kampeni zao za hadhara au kuzuru wapiga kura kwenye majumbani mwao.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kwamba kuanzia kati ya mwezi Julai, wahamiaji wa ndani (IDPs) 765,000 katika Pakistan - sawa na asilimia 33 ya jumla ya IDPs - walisajiliwa kurejea makwao, hali ambayo ilisababisha UM kufunga kambi nne za makazi ya muda. Lakini vile vile, kwa sababu ya mapigano yaliopamba kwenye wilaya ya Dir ya Juu, Ofisi ya UM juu ya Huduma za Wahamiaji imeripoti kulazimika kuanzisha kambi mpya za makazi ya muda. Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) pamoja na UNHCR zinashirikiana sasa hivi kuanzisha vituo vinne vya ugawaji wa huduma za kimsingi pamoja na ugawaji wa chakula kwa wale wahamiaji wanaorejea makwao. Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo (UNICEF) imo mbioni kuzifanyia matengenezo skuli 100 zilizoharibiwa na vurugu na mapigano. Wakati huo huo Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) limemaliza tathmini ya uharibifu uliojiri kwenye eneo la uhasama na mapigano, na limeripoti mavuno ya nafaka, matunda na mbog yameharibiwa vibaya sana kwenye eneo husika. OCHA imethibitisha Mradi wa Misaada ya Dharura kwa Pakistan umefanikiwa kupokea asilimia 44 ya msaada wa fedha uliogharamiwa dola milioni 542, mchango unaohitajika kuhudumia kihali waathirika husika.