Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti mashirika ya UM yanayohudumia misaada ya kihali yalishindwa mwezi Julai kuwafikia watu 500,000 wenye njaa katika Usomali, na kuwapatia chakula. Ripoti ilisema idadi hiyo ni miongoni mwa raia milioni 3.3 wa Usomali wenye kutegemea kufadhiliwa chakula na jamii ya kimataifa, hususan wale raia waliopo kwenye mji mkuu wa Mogadishu na katika eneo la kusini kuliposhtadi mapigano kwa wingi. Wakati huo huo Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetangaza ya kuwa kuanzia Oktoba, litakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula cha kugawia watu muhitaji kimataifa. WFP ilisema itahitaji kufadhiliwa tani za metriki 209,000 za chakula, zinazogharamiwa dola milioni 208, kuweza kukidhi mahitaji ya chakula ya umma wa kimataifa katika kipindi cha sasa hivi hadi mwisho wa Machi 2010.

KM Ban Ki-moon ametoa mwito wa dharura kwenye kikao cha hadhara asubuhi ya leo, unaolitaka Baraza la Usalama kubuni tume huru ya uchunguzi wa kupeleleza vitendo vya unyanyasaji wa kijinsiya katika maeneo ya mizozo iliopamba kwenye mataifa ya Chad, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Sudan. Alisema kutokana na ripoti alizopokea imegundulikana wapiganaji kwenye mataifa hayo matatu ya Afrika hujihusisha kwenye vitendo vya kutumia mabavu ya kunajisi wanawake kihorera, kuwa kama ni silaha ya vita, ambayo huitumia kwa "ustadi katili", sawa na bunduki au vijikombora vya grenedi. KM alipendekeza tume hiyo isaidiwe na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, na ichukue jukumu la kupendekeza kwa Baraza la Usalama "utaratibu madhubuti unaofaa kuchukuliwa kuhakikisha wakosa wa jinai iliovuka mipaka ya kunyanyasa na kudhalilisha wanawake kihorera huwa wanafikishwa mahakamani kupata adhabu." Aliyasema haya mbele ya wajumbe 15 wa Baraza laUsalama walipokuwa wanazingatia masuala ya "usalama, amani na hifadhi ya wanawake kwenye mizozo".

KM amekaribisha kwa ridhaa kuu mkutano wa uliofanyika Alkhamisi (06/08/2009) kwenye mji wa Goma, katika JKK, baina ya Raisi wa Rwanda Paul Kagame na Raisi Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kideomkrasi ya Kongo uliokusudiwa kurudisha amani kwenye eneo lao. Mkutano huu ni wa kwanza ambapo viongozi wawili hawa wawili walipata fursa ya kuonana uso kwa uso, kufuatia mazungumzo yao kama haya yaliofanyika 1996. KM alifurahika na ahadi waliotoa kipamoja iliosisitiza kuwepo kwa haja ya dharura inayotakikana kuimarisha kihakika "utulivu na amani katika eneo la Maziwa Makuu."

Michel Sidibé, Mkurugenzi Mkuu wa Jumiya ya Mashirika ya UM Kukabiliana na UKIMWI (UNAIDS) amepongeza mapatano yaliofikiwa na Waqf wa Clinton (Clinton Foundation) na kampunzi za kimataifa za kutengeneza madawa za Pfizer na Matrix kupunguza bei za dawa za kurefusha maisha wanazopewa wagonjwa wenye kuishi na virusi vya UKIMWI na kifua kikuu (TB). Alisema hatua hii itanusuru maisha ya wagonjwa milioni 4 wa UKMWI na TB waliopo ulimwenguni, na utasaidia kusarifia miradi ya matibabu ya kitaifa ya muda mrefu. Kwa mujibu wa taarifa za WHO dawa za kurefusha maisha ni muhimu kwa wale wagonjwa wa UKIMWI wasioweza kutibika na tiba ya awali inayotakikana kudhibiti mapema maradhi haya, wagonjwa ambao UM inakadiria idadi yao inakaribia milioni thelathini na tatu.