Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulio ya raia Sudan Kusini yamelaaniwa na BU

Mashambulio ya raia Sudan Kusini yamelaaniwa na BU

Ijumanne alasiri wajumbe wa Baraza la Usalama [BU] walilaani, kwa kauli ya pamoja, "mashambulio karaha" yaliotukia mwisho wa wiki iliopita Sudan kusini, ambapo inakadiriwa watu 185 waliuawa, wingi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo.

Raisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Agosti, Balozi John Sawers wa Uingereza, kwenye risala alioiwakilisha kwa waandishi habari, alisema tukio la Sudan kusini limeitia wasiwasi mkuu jumuiya ya kimataifa, kwa sababu mashambulio yalifanyika kwa kutumia silaha za kisasa na yaliwalenga zaidi wanawake na watoto. Balozi Sawers, ambaye alizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Baraza la Usalama, alikumbusha tena ni wajibu wa wenye madaraka kuhakikisha raia huwa wanapatiwa hifadhi inayoridhisha dhidi ya mashambulio ya kikatili, na pia kuhakikisha waathirika wa misiba kama hiyo huwa wanapatiwa misaada ya kihali kukidhi mahitaji yao ya kimsingi.