Taarifa mpya ya WHO kuhusu A/H1N1

Taarifa mpya ya WHO kuhusu A/H1N1

Shirika la Afya Duniani (WHO) leo limetangaza kutoka Geneva, takwimu mpya kuhusu maambukizo ya homa ya mafua ya A/H1N1 katika dunia.

Ripoti ilisema jumla ya watu 162,380 walithibitishwa na maabara za afya, katika nchi 168, kuwa waliambukizwa na homa ya mafua ya H1N1, katika kipindi kilichomalizikia tarehe 31 Julai 2009. Kadhalika, WHO imeeleza jumla ya vifo vilivyosajiliwa kimataifa kutokana na homa ya mafua ya H1N1 ni sawa na vifo 1,154 na mataifa yenye kuongoza ni yale mataifa ya Amerika ambapo watu 1,008 walisajiliwa kufariki kwa sababu ya kupatwa na maradhi ya homa ya mafua ya H1N1. Kwa mujibu wa WHO, sasa hivi janga la maambukizi ya homa hii limegundulikana, takriban katika mabara yote ya ulimwengu; na wakati huo huo kumegunduliwa karibuni aina ya virusi sugu vya homa ya H1N1 miongoni mwa wagonjwa sita, waliokutikana katika mataifa ya Denmark, Ujapani, Kanada na Jimbo la Hong Kong, Uchina. Wagonjwa watatu wa kundi hilo walikuwa kutoka Ujapani. Dktr Keiji Fukuda, Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa WHO alibashiria, kwenye taarifa yake ya karibuni, kwamba watu bilioni 2 huenda wakaambukizwa na janga la homa ya mafua ya H1N1 kabla tatizo hili halijadhibitiwa kikamilifu katika siku zijazo.