Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Tiébilé Dramé, mshauri mkuu wa UM juu ya masuala ya kisiasa ya Bukini ameripotiwa kuwa miongoni mwa wapatanishi waliokusanyika Ijumatano kwenye mji mkuu wa Maputo, Msumbiji kusimamia mazungumzo ya kusuluhisha mzozo wa kisiasa uliojiri Bukini kwa muda mrefu sasa. Juhudi hizi za upatanishi zinafanyika kwa niaba ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na kuongozwa na Raisi mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano. Kadhalika mazungumzo yamejumuisha wawakilishi wa kutoka Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na wanachama wa Jumuiya ya Wazungumzaji Kifaransa (Francophonie).

Rodolphe Adada, Mjumbe Maalumu wa Pamoja wa Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) alikutana Ijumatano na wawakilishi wa kambi ya wahamiaji wa ndani (IDPs) ambao wiki iliopita kiongozi wao pamoja na mkewe waliuawa. Adada alizungumza na wawakilishi hawa wa IDPs juu ya hatua za kuchukuliwa kuimarisha hifadhi ya wahamiaji kwenye makazi yao ya muda. Kadhalika, aliwahimiza wakazi wa kambi za IDPs kushirikiana na UNAMID kwa kuwapatia taarifa zinazohitajika kuhakikisha usalama wao, na vile vile kuwataka wazipe umuhimu unaostahiki kazi za ulinzi wa jamii. Viongozi wa kambi za wahamiaji wa IDPs wanatarajiwa kuzingatia mapendekezo hayo kwa ushauri na Polisi wa UNAMID.

Kadhalika, UNAMID imetangaza askari walinzi amani wa Ethiopia 151 wamewasili Darfur na wanajeshi 151 ziada watawasili huko kesho Alkhamisi. Walinzi amani wa Ethiopia wanatazamiwa kukamilisha jumla ya askari 1400 ziada watakapokamilisha kuenezwa katika Darfur katika mwezi Septemba. Kwa kulingana na taarifa hiyo, Mpatanishi Mkuu wa Pamoja kwa Darfur, Djibril Bassolé, yupo Libya hivi sasa ambapo anakutana na makundi kadha ya Darfur, yaliopendekeza kushiriki kwenye mazungumzo ya amani na Serikali ya Sudan. UNAMID imeripoti usalama katika Darfur kwa sasa ni shwari, isipokuwa kwa vitimbi vya maharamia ambavyo vinaendelea kuzuka hapa na pale kwenye eneo.

Shirika la UM la Kulinda Amani katika JKK (MONUC) limeripoti ya kwamba tangu mwezi Februari mwaka huu, lilipeleka kwenye eneo la mashariki la Jimbo la Kivu, timu 40 za maofisa wanaohusika na huduma za kuhifadhi raia. Timu hizi ziliandaliwa mnamo mwanzo wa mwaka, na zilijumlisha maofisa wataalamu juu ya hifadhi ya watoto na masuala ya kiraia, pamoja na wale maofisa wanaoshughulikia habari za umma. Maofisa hawa watasaidia kutambua na kuhadharisha mapema ishara za kuzuka mazingira yenye kuhatarisha raia, hali ambayo itayaruhusu wanajeshi kuelekea kwenye eneo husika kwa mapema na kuidhibiti haraka. Kadhalika, MONUC imetuma ujumbe maalumu kwenye eneo la mashariki, kwa madhumuni ya kusailia hatua kinga dhidi ya udhalilishaji wa kijinsiya na unyanyasaji wa wanawake ambao, baadhi ya nyakati, huendelezwa na wanajeshi wa kulinda amani wa UM. MONUC inatarajiwa kutoa ripoti juu ya suala hilo katika siku za karibuni.