Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umeitisha kikao maalumu Bonn kuhamasisha maafikiano ya Mkutano wa Copenhagen

UM umeitisha kikao maalumu Bonn kuhamasisha maafikiano ya Mkutano wa Copenhagen

Imetangazwa kwamba UM karibuni utafanyisha kikao, kisio rasmi, cha mashauriano, kuzingataia taratibu za kuimarisha zaidi hatua za utendaji za ule waraka wa kujadiliwa mwezi Disemba, kwenye Mkutano wa Copenhagen wa kudhibiti bora taathira za mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.

Mashauriano haya yatafanyika katika mji wa Bonn, Ujerumani kuanzia tarehe 10 mpaka 14 Agosti 2009. Kama inavyofahamika, Muafaka wa Copenhagen utafuatia awamu ya awali ya utekelezaji wa Mkataba wa Kyoto, ambao muda wake utamalizika mnamo 2012. Yvo de Boer, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya UM ya juu ya Utendaji wa Mkataba wa Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani (UNFCCC) ameripotiwa akisema wajumbe wa kimataifa sasa hivi wamefikia "kipindi cha kusisimua" kwenye majadiliano yao juu ya ajenda ya Copenhagen, majadiliano ambayo yanaonyesha dalili za kutia moyo, zinayoongoza Mataifa Wanachama "kwenye kipindi muhimu cha mageuzi katika kupiga vita na kudhibiti athari haribifu za mabadiliko ya hali ya hewa" katika ulimwengu.