Skip to main content

Kamishna wa Haki za Binadamu aingiwa wahka na ripoti za fujo Nigeria

Kamishna wa Haki za Binadamu aingiwa wahka na ripoti za fujo Nigeria

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay, ametangaza hii leo kutoka Geneva ya kwamba ana wahka mkubwa kuhusu ripoti alizopokea, juu ya taathira za kufumka kwa vurugu ikichanganyika na hali mbaya ya raia iliotanda majuzi katika eneo la Nigeria kaskazini, kufuatia mashambulio ya wafuasi wa kundi la kidini linaloitwa ‘Boko Haram\'.

Jambo linamlotia wasiwasi Kamishna Mkuu Pillay, ilisema taarifa, ni yale mauaji ya kihorera ya raia yaliotukia wakati wa mapigano, pamoja na vitendo vya kuwakamata watu kwa wingi na kuwaweka vizuizini, na pia tatizo la umma kung'olewa makazi, wakati raia wengine wakilazimika kuyakimbia mastakimu yao na kuelekea kwenye kambi za wanajeshi kupata hifadhi. Pillay alisema anafahamu Serikali ya Nigeria, kwa sasa, imekabiliwa na mgogoro mkuu ambapo mapigano yalishtadi kwenye vitivo vya miji mikuu ya majimbo. Alisema anatumai Serikali itachukua kila hatua, zitakazohakikisha utulivu na usalama unarejeshwa kwenye maeneo ya mzozo, kwa utaraibu utakaotekeleza kikamilifu uhalali wa sheria na kuhishimu haki za binadamu, halkadhalika. Alisisitiza kwamba Serikali inawajibika kufanya kila bidii yenye kuhakikisha itajiepusha na mauaji nje ya sheria, na pia kuisihi Serikali ijitahidi kukwepa tabia ya kushika watu na kuwatia vizuizini kihorera. Pillay, alitoa mwito uitakayo Serikali ya Nigeria kufanya ukaguzi wa kuridhisha kuhusu matukio yote yanayoambatana na vurugu na, baadaye, kuwafikisha mahakamani wale waliowajibika na fujo hizo ili kukabili sheria. Kamishna Mkuu wa Haki za Bindamu, Navi Pillay aliwatumia mkono wa pole aila zote za waathirika wa vurugu pamoja na majeruhi.