Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Baraza la Usalama Ijumanne limepitisha, kwa kauli moja, azimio 1882 (2009) liliolaani, kwa kauli nzito, wale watu na makundi yenye kutengua sheria ya kimataifa wanapowalazimisha watoto wadogo kushiriki kwenye mapigano. Azimio limetoa mwito maalumu wenye kumtaka KM Ban Ki-moon aongeze kwenye orodha ya wakosa wa uhalifu wa kuajiri watoto kwenye mapigano, vile vile yale majina ya watu wenye kuua watoto wadogo na kuwalemaza, pamoja na watu wanaonajisi watoto kimabavu kwenye mazingira ya mapigano na vita. Orodha hii ya KM inajulikana kama “orodha ya izara/fedheha”. Azimio la Baraza la Usalama liliwataka wale wote waliomo kwenye orodha kutayarisha “mipango ya utendaji, ya muda maalumu, kukomesha haraka vitendo vyao na matumizi mabaya ya watoto.” Kadhalika, Baraza la Usalama “limeyataka Mataifa Wanachama husika kuchukua hatua za dhahiri, na za dharura, dhidi ya watu wanaoendelea kukiuka sheria ambao hukandamiza watoto kwenye mazingira ya mapigano”. Mataifa Wanachama yanatarajiwa kuwafikisha wakosa hawa mahakamani kukabili mashtaka kwa kuvunja sheria dhidi ya utunzaji na hifadhi ya watoto.

Mkuu wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) amenakiliwa akisema makundi ya kidini ni taasisi muhimu katika kusukuma mbele shughuli za maendeleo. Alisisitiza ya kuwa UM unawajibika kukuza ushirikiano wake maalumu na jumuiya hizi za kidini, kwa lengo la kuimarisha zaidi masilahi ya umma ulio dhaifu kihali na mali. Mkurugenzi Mkuu wa UNFPA, Thoraya Ahmed Obeid aliwaambia wajumbe walioshiriki kwenye mazungumzo ya "meza ya mzunguko" na jumuiya za kidini, yaliofanyika kwenye jiji la New York Ijumatatu, kuwa taasisi yao imeshatambua kitambo "madaraka ya kimaadili walionayo viongozi wa kidini" na pia imethibitisha "ukweli wa kuwa mashirika ya kidini ndio jumuiya kongwe kabisa za wanadamu zilizokuwa zikitoa huduma za kijamii kihistoria." Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) na Benki Kuu ya Dunia, baina ya asilimia 30 mpaka 60 ya huduma za afya ya msingi zinazotolewa katika nchi zinazoendelea, husimamiwa na kuongozwa na jumuiya za kidini. Kadhalika, taarifa iliongeza kusema, kwenye baadhi ya sehemu hizo huduma za ilimu na afya zinazotolewa na mashirika ya kidini ni bora zaidi kushinda zile zinazotolewa na serikali.

Ijumanne, Baraza la Usalama limeafikiana juu ya mada za kuzingatiwa kwenye vikao vyake vya Agosti, vitakavyongozwa na Balozi wa Uingereza katika UM John Sawers. Alasiri Baraza la Usalama lilifanyisha kikao cha hadhara, kuzingatia ripoti mpya ya KM kuhusu shughuli za Shirika la UM Kusaidia Amani Iraq (UNAMI). Kadhalika, kwenye kikao kingine cha faragha Baraza la Usalama lilizingatia ripoti kuhusu Sudan na operesheni za amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Ripoti hizi ziliwasilishwa na Alain Le Roy, Naibu KM juu ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM Duniani.

Kundi la awali wanajeshi wa amani 134 kutoka Burkina Faso limewasili Darfur Ijumanne kujiunga na Vikosi vya Mchanaganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID). Wanajeshi hawa wataenezwa kwenye eneo la karibu na El Geneina, mji mkuu wa Darfur Magharibi, na katika Foro Baranga, eneo liliopo kilomita 300 kutokea El Geneina. Kadhalika, wanajeshi ziada 133 wa Burkina Faso wanatazamiwa kuwasili Darfur wiki ijayo. Walinzi Amani wa Burkina Faso watakapokamilisha mchango wao kwa UNAMID mwezi Septemba, idadi yao itazidi wanajeshi 800, ambao hujumuisha vile vile waangalizi wa kijeshi, maofisa wa jeshi na maofisa wa ushirikiano.