Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO inasailia kitendawili cha suala lipi la afya lastahili misaada ya kimataifa

WHO inasailia kitendawili cha suala lipi la afya lastahili misaada ya kimataifa

Jarida la Shirika Afya Duniani (WHO) liliochapishwa Geneva, siku ya leo, limeeleza kwamba masuala ya afya ya jamii hupewa umuhimu na viongozi wa kisiasa, wafadhili wa kimataifa na pia jumuiya za kiraia, kwa kutokana na namna matatizo haya yanavyojulishwa, kutangazwa na kuenezwa.

Profesa Jeremy Shiffman, wa kutoka Kitivo cha Maxwell cha Chuo Kikuu cha Syracuse, katika Jimbo la New York, Marekani alinakiliwa na WHO akisema kwamba kwa tatizo la afya ya kimataifa kufanikiwa kupatiwa msaada wa fedha unaostahiki, au kuripotiwa kimataifa kama inavyotakikana, hutegemea zaidi namna suala hilo linavyoelezewa au kusimuliwa na vyombo vya mawasiliano badala ya ukweli ulivyo juu ya "umuhimu halisi" wa suala hili. Alizisihi jamii za kimataifa kwamba zikitaka kufanikiwa kufadhiliwa misaada maridhawa ya fedha na wahisani wa kimataifa na kuhakikisha matatizo yao ya afya yatavuta usikizi mkubwa zaidi pindi watawajibika kuonyesha suala hilo kuwa ni sio tatizo la afya ya jamii pekee bali ni tatizo linalohatarisha kimsingi afya na ustawi wa wanadamu, usalama wa kitaifa na pia maendeleo ya kiuchumi na jamii.