Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umma wa Niger wanasihiwa na KM kuonyesha uvumilivu kwenye upigaji kura ya maoni kurekibisha katiba

Umma wa Niger wanasihiwa na KM kuonyesha uvumilivu kwenye upigaji kura ya maoni kurekibisha katiba

KM Ban Ki-moon, kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wake, juzi ametoa nasaha maalumu kwa umma wa Niger kujizuia na machafuko na vurugu nchini mwao, na kuutaka pia umma uonyeshe uvumilivu wa hali ya juu wakati wanajiandaa kushiriki kwenye kura ya maoni, yenye utata, ambayo lengo lake hasa ni kubadilisha katiba itakayomruhusu Raisi wa sasa kugombania uchaguzi kwa mara ya tatu.

 KM alisema anaunga mkono "utaratibu wa kutatua mzozo uliojiri nchini, juu ya kura ya maoni, utakaojumuisha kila raia, kwa kuambatana na mifumo ya kidemokrasia, ili kuhakikisha mvutano wao utasulushishwa kwa njia ya amani." Niger imeitisha kura ya maoni nchini, Ijumanne, tarehe 04 Agosti, kuidhinisha marekibisho ya katiba yatakayomruhusu raisi kuwepo madarakani kwa muda zaidi, na kumwezesha raisi wa hivi sasa, Mamadou Tandja kugombania madaraka kwa mara ya tatu mfululizo. KM alisema ana wasiwasi kura ya maoni hiyo inafanyika "licha ya kuwepo tofauti kali za maoni baina ya wadau wote husika." Taarifa ya KM imeahidi kuwa UM upo tayari kuisaidia Niger kusuluhisha, kwa amani, mkwaruzano wa kisiasa ulioibuka nchini, kwa kuhakikisha utulivu unadumishwa kieneo."