Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Uingereza imechukua madaraka ya uraisi wa duru wa Baraza la Usalama kwa mwezi Agosti, kwa mujibu wa taarida za Msemaji wa KM. Raisi wa Baraza, Balozi John Sawers wa Uingereza alikuwa na mashauriano kadha wa kadha na wajumbe wa taasisi hiyo ambao walizingatia ajenda ya kazi kwa mwezi huu.

Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) kwenye ripoti iliotoa karibuni, limeeleza hali ya usalama, kwa ujumla, kwenye eneo la operesheni zao ni shwari, isipokuwa kwa matukio madogo ya ujambazi na wizi wa magari yalionekana kuzuka Darfur Kaskazini. Shirika la UNAMID limearifu pia kwamba Naibu Mjumbe Maalumu wa Pamoja kwa Darfur, Henry Anyidoho, Ijumapili alizuru kambi ya wahamiaji wa ndani ya Kalma, karibu na Nyala, Darfur Kusini. Anyidoho alipokuwepo huko alifanya ukaguzi wa maendeleo ya shughuli za wahandisi wa UNAMID waliokuwa wakihudumia misaada ya kihali kieneo baada ya mafuriko makubwa kutukia karibuni Darfur Kusini. Kadhalika, Anyidoho alikutana na viongozi wa kimila ambao alikuwa na mashauriano nawo juu ya huduma wanazopatiwa wahamiaji wa ndani na jumuiya ya kimataifa, kwenye kambi ya Kalma, na walizingatia pia uwezekano wa kuwarudisha makwao, kwa khiyari, baadhi ya raia waliotayari kufanya. Aliwapatia wawakilishi wa jumuiya za kiraia, za kizalendo, mchango wa dola 250,000, kwa niaba ya UNAMID, zitakazotumiwa kujengea madarasa, vyoo na mabomba ya maji katika kambi ya Kalma. Wakati huo huo, kuanzia Ijumamosi ya tarehe 01 Agosti imeripotiwa na UM kwamba vikosi vya UNAMID vilianzisha doria za mchana kutwa katika kambi 14 za wahamiaji ziliopo kwenye jimbo zima la Darfur. Upanuzi wa doria hizi umeanzishwa baada ya kuwasili washauri wa polisi 36 kutoka Malawi. Vile vile UNAMID inatarajia wiki hii kuwasili polisi 80 ziada kutoka Afrika Kusini ambao watashirikiana na polisi wa Malawi kuimarisha usalama kwenye kambi za wahamiaji wa ndani wa Darfur.

Tunzo ya Kimataifa ya Ujuzi wa Kusoma na Kuandika kwa 2009, inayotolewa kila mwaka na Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) imetunukiwa gazeti la kijiji cha Bara Hindi ambalo huendeshwa na wanawake peke yao. Kadhalika Zawadi ya UNESCO imetunukiwa miradi mitatu ya ubunifu wa kisasa wa kusoma na kuandika, inayotekelezwa kwenye mataifa ya Afghanistan, Burkina Faso na Philippines. Hali kadhalika, Mradi wa Masomo Usio-Rasmi, unaoongozwa na Wizara ya Ilimu ya Bhutan ulipatiwa hadhi ya kuhishimwa na UNESCO kwa kutambuliwa kuwa inatumia utaratibu wa jumla, kusimamia mradi wa kujua kusoma na kuandika.

Ann Veneman, Mkurugenzi Muu wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) amekamilisha ziara yake katika Nigeria Kaskazini, ambapo alifadhilia msaada ziada wa dola milioni 1.85 utumiwe kuimarisha miradi ya lishe bora kwenye eneo hilo. Msaada huu utatumiwa kwenye miradi inayounganisha pamoja vituo vya jumuiya vinavyoshughulikia huduma za lishe, ambapo watu hupeleka watoto wao kupatiwa huduma kinga na tiba dhidi ya matatizo ya utapiamlo na hali kama hiyo. Wakati alipokuwa Nigeria, Veneman pia alikutana na wakuu wa serikali pamoja na viongozi wa kidini, na kujadiliana nawo haja kuu ya kufyeka kabisa maradhi ya kupooza/polio nchini. Nigeria ni miongoni mwa mataifa manne ulimwenguni ambayo polio bado imesalia, na ni taifa pekee katika Afrika ambapo maradhi ya kupooza yameselelea. Veneman alitangaza UNICEF kuwa itachangisha dola milioni 5 zaidi kuisaidia Nigeria kuondosha kabisa maradhi ya kupooza katika nchi.

Robert Serry, Mratibu Maalumu wa UM kwa Mpango wa Amani Mashariki ya Kati, ameripotiwa kulaani, kwa kauli nzito, kitendo cha vikosi vya usalama vya Israel cha kuwang'oa kimabavu, aila kadha za KiFalastina, kutoka majumbani mwao, kwenye mitaa ya WaArabu ya Sheikh Jarrah iliopo Jerusalem Mashariki. Alisema vitendo hivi ni "visokubalika kisheria asilan", hasa ilivyokuwa mali halali ya WaFalastina imekabidhiwa walowezi wa Kiisrael na kuwalazimisha wenye mali WaFalastina kusajiliwa kama wahamiaji na Shirika la UM la Kufarajia Wahamiaji wa KiFalastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA). Serry alikumbusha kitendo cha kuwatoa kimabavu WaFalastina wa Sheikh Jarrah majumbani mwao, na kuwapokonya mali zao, kinaharamisha Mkataba wa Geneva juu ya hifadhi ya watru wanaokaliwa na taifa la kigeni, na ni kitendo chenye kupuuza, vile vile, ule mwito wa jumuiya ya kimataifa unaoitaka Israel kujizuia na vitendo vya uchokozi katika eneo la Jerusalem Mashariki. Sherry alisema hakubaliani na madai ya Israel ya kuwa hatua ilizochukua zinahusiana na shughuli za mamlaka ya manispaa na mahakama za nchi pekee! Serry aliitaka Israel kutekeleza sheria ya kimataifa, pamoja na majukumu ilioidhinisha kwenye Ramani ya Mpango wa Amani kwa kusitisha na kubadilisha uamuzi wake huo. Ijumatatu, UNRWA imeshiriki kuwasaidia wahamiaji waliofukuzwa makwao kupata mali na vitu vyao vya nyumba ambavyo vilitiwa kwenye malori ya wenye madaraka Israel, na baadaye kutupwa kwenye eneo la magugu karibu na ukingo wa njia kuu ya Jerusalem, iliojaa magari mengi, barabara inayojulikana kwa umaarufu kama Route One. Vitu na vikorokoro vya WaFalastina waliong'olewa mastakimu sasa hivi vimewekwa kwenye maghala ya UNRWA. Kwa mujibu wa UNRWA familia zilizofukuzwa kwenye nyumba zao walikuwa wakiishi humo kwa miaka zaidi ya nusu karne, na wingi wao wamepigwa na mshtuko mkubwa na kihoro kisio kifani. Jumla ya watu waliofukuzwa majumbani mwao ni 53, na kati ya jumla hiyo kuna watoto wadogo 20 ambao UNRWA inasema ndio walioathirika zaidi kiakili.