Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama Alkhamisi limepitisha azimio la kuongeza muda wa operesheni mbili za UM juu ya ulinzi amani katika Cote d\'Ivoire na Darfur, Sudan. Kuhusu Cote d\'Ivoire Baraza lilipiga kura kwa kauli moja kuongeza kwa miezi sita muda wa operesheni za Shirika la UM Kulinda Amani katika Cote d\'Ivoire (UNOCI). Wakati huo huo Baraza limeidhinisha kibali cha kibali cha kuendeleza operesheni za Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) kwa miezi kumi na mbili ijayo, hadi Julai 2010. Kadhalika Baraza la Usalama lilimtaka KM atayarishe mradi wa utendaji wenye vigezo vya kutathminia na kufuatilia maendeleo juu ya namna maazimio ya Baraza yanatekelezwa katika Darfur.

Josette Sheeran, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP), ambaye wiki hii anazuru Washington D.C. Marekani alinakiliwa akisema taasisi yao sasa hivi inakabiliwa na upungufu mkubwa wa kihistoria, na ulio wa hatari kuhusu misaada inayofadhiliwa na wahisani wa kimataifa. Alibainisha ya kuwa jumla ya fedha zinazohitajika kuendesha shughuli zake kwa mwaka huu ni dola bilioni 6.7, na matarajio ya WFP ni kuwa ikibahatika itapokea dola bilioni 3.7 kuhudumia chakula watu milioni 108 wenye kuishi katika nchi masikini sabini na nne. Alisema baada ya kukamilisha nusu mwaka, mchango uliothibitishwa kukusanywa kutoka wafadhili wa kimataifa kwa sasa ni sawa na dola bilioni 1.8, hali ambayo imeilazimisha WFP kupunguza posho ya chakula kwa ule umma muhitaji wa kimataifa, na hata kulazimika kusimamisha huduma za kugawa chakula katika baadhi ya nchi kwa sababu ya upungufu wa fedha.

Naibu Mkurugenzi wa UM juu ya Huduma za Dharura, Catherine Bragg Alkhamisi amekamilisha ziara yake katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (JAK).Kwenye mahojiano aaliokuwa nayo na waandishi habari kwenye mji mkuu wa Bangui, alisisitiza kwamba mzozo wa masuala ya kiutu nchini humo hautokani na mafuriko ya mizozo ya mataifa jirani pekee. Bragg alisema licha ya kuwa maendeleo fulani yalipatikana juu ya huduma za kiutu nchini, hata hivyo hali nchini ni bado ya kubadilikabadilika na ni ya hatari, wakati raia waliong'olewa makazi wanaendelea kubainisha dalili za kudhurika na kihoro na kiwewe. Aliwaomba wenye madaraka kutekeleza majukumu yao ya kuwalinda raia, na kuhakikisha watumishi wanaohudumia misaada ya kiutu wanaruhusiwa kuendeleza shughuli zao za kuwafikia raia muhitaji, bila pingamizi.

Ripoti ya KM kwa Baraza la Usalama juu ya mapitio ya utekelezaji wa maazimio yake katika Iraq, iliotolewa leo Alkhamisi, imeorodhesha masuala kadha yaliosalia na ambayo yanayohitajia suluhu ya mapema, hususan lile suala la uhusiano wa Iraq na Kuwait. Kwenye ripoti KM alikumbusha Iraq inajitahidi kuibuka, kwa polepole, kutoka yale mazingira magumu ambapo Iraq ilikabiliwa na vita kuu mbili. KM alisema anaelewa vyema kwa nini umma wa Iraq unasisitiza ukabidhiwe mamlaka kamili ya taifa, na kurudishiwa haki yao halali ya kujiunga tena na jumuiya ya kimataifa. KM aliitaka Iraq na Kuwait kujaribu ya kuzingatia hatua bunifu za kutatua matatizo yaliosalia kati yao, kwa maadili ya ukarimu wa maelewano juu ya wasiwasi na khofu zinazowasumbua kitaifa.

UM umeripoti mnamo siku ya leo, kwenye eneo la pwani ya Ghaza ya kaskazini, maelfu ya watoto wa KiFalastina walishiriki kwenye tukio la kurusha vishada, kwa madhumuni ya kuvunja Rikodi ya Dunia ya Guinness, inayohusu jumla ya vishada vinavyopeperushwa angani kwa wakati mmoja. Tukio hili ilikuwa ni mojawapo ya mradi wa Michezo ya Riadha kwa Majira ya Kiangazi, mradi unaosimamiwa na Shirika la UM Linalofarajia Misaada ya Kiutu kwa Wahamiaji wa KiFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA). Michezo hii, ambayo imetimiza miaka mitatu tangu kuanzishwa, huwapatia watoto 240,000 fursa ya kushiriki kwenye riadha, kutengeneza sanaa ya kazi za mkono, pamoja na futsa ya kujihusisha na maonyesho ya tamthilia na vile vile huwapatia masomo ya kujirekibisha. Kwa mujibu wa UNRWA kadhia hizi huwasaidia watoto wanaoishi katika Tarafa ya Ghaza, kwenye mazingira ya wasiwasi, kupata hisia za kuwa na maisha ya kawaida na kuwarudishia hadhi yao ya kiutu, mchango ambao una thamani kubwa katika huduma za kuimarisha amani kwenye eneo husika la Mashariki ya Kati.