Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO itafadhiliwa dola milioni 2.5 na Saudi Arabia kutayarisha mkutano wa kukomesha njaa

FAO itafadhiliwa dola milioni 2.5 na Saudi Arabia kutayarisha mkutano wa kukomesha njaa

UM umetangaza ya kuwa Saudi Arabia itafadhilia msaada wa dola milioni 2.5 kwa Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) ili kuiwezesha taasisi hii kufanyisha Mkutano Mkuu juu ya Udhibiti Bora wa Akiba ya Chakula Duniani, utakaojumuisha wajumbe kadha wa kadha wa kutoka Mataifa Wanachama kwenye Makao Makuu ya FAO mjini Roma, Utaliana kuanzia tarehe 16 hadi 18 Novemba mwaka huu.

Lengo la kikao kijacho cha FAO ni kuhamasisha Mataifa kuchangisha misaada rasmi ya mendeleo ya kilimo, itakayolingana na kima cha misaada iliyofadhiliwa katika 1980, ambapo asilimia 17 ya misaada hiyo iliekezwa kwenye huduma za kilimo. Kadhia hii ikitekelezwa, ilieleza FAO, itasaidia zile juhudi za kukomesha matatizo ya njaa sugu, ambayo sasa hivi husumbua hali za watu bilioni moja katika ulimwengu. Kadhalika mchango huo rasmi ukikamilishwa unatarajiwa kuongeza maradufu uzalishaji wa kilimo na, hatimaye, kuwawezesha walimwengu kuhudumia chakula umma unaokadiriwa kufikia watu bilioni 9 katika 2050.