Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM kuisaidia Angola kuhudumia raia maji safi

UM kuisaidia Angola kuhudumia raia maji safi

Mradi wa Pamoja wa Mashirika ya UM Kuhudumia Maji na Usafi umeanzishwa rasmi karibuni nchini Angola.

Mpango huu wa kuimarisha maendeleo, unaotambuliwa kwa umaarufu kama "Mradi wa Maji Safi kwa Wote", ulianzishwa wiki iliopita kwenye mji mkuu wa Luanda, Angola na umekusudiwa kuwapatia maji safi ya matumizi, kwa asilimia 80 ya wakazi wa kwenye miji nchini humo, na vile vile kuhudumia maji safi asilimia 50 ya wanavijiji itakapofika mwaka 2020. Mradi huu wa miaka mingi unatokana na uamuzi wa pamoja wa Serikali ya Angola, Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF); mashirika ya UM juu ya Maendeleo (UNDP) na haki za wafanyakazi (ILO), pamoja na taasisi isio ya kiserikali, ya kizalendo, inayioshughulikia tiba na madawa. Kwa mujibu wa taarifa za UM, maji safi ya mifereji na mabomba ni ghali sana kwa raia wa kawaida waishio Angola, hali ambayo mara nyingi huwalazimisha raia hawa kutegemea maji yasio salama, ambayo ikichanganyika na ukosefu wa mazingira safi huchochea asilimia 90 ya vifo vinavyosababishwa na maradhi ya kuharisha. Shirika la UNICEF limekumbusha ya kuwa kila mtoto ana haki ya kuwa na uwezo wa kuishi kwenye mazingira safi na kupatiwa maji salama yatakayokinga afya bora, kama ilivyoidhinishwa ndani ya Mkataba wa Haki za Mtoto.