Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) liomeripoti Kamisheni ya Uchaguzi wa Taifa Sudan imewaarifu ya kuwa imeshakamilisha kuweka mipaka ya maeneo ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwezi Aprili 2010. Vile vile Kamisheni ilisema imeshaanzisha kamati tatu zitakazoshughulikia upigaji kura kwenye majimbo yote matatu ya Darfur. Taarifa ya Kamisheni ya Uchaguzi wa Taifa Sudan pia ilisema makundi ya kiraia yataruhusiwa kuendeleza shughuli za kuhamasisha wapiga kura kutekeleza haki zao za kimsingi, bila ya kuingiliwa kati na serikali, hususan kutoka zile idara za usalama na ulinzi au ile Kamisheni juu ya Misaada ya Kiutu, na walihakikishiwa masuala yote yenye mvutano yatapelekwa kusailiwa na Kamisheni ya Uchaguzi.

Wawakilishi Wakazi wa Timu ya UM Wanaohudumia Misaada ya Kiutu katika Maeneo Yaliokaliwa ya WaFalastina (OPT) - ambao huwakilisha mashirika ya UM - na vile vile hujumlisha watumishi wa mashirika ya kimataifa juu ya maendeleo, Ijumanne walifanyisha tukio maalumu kwa dhamira ya kutetea haki za watoto wa KiFalastina waliodhurika kiakili na kimwili katika Tarafa ya Ghaza, kufuatia mashambulio ya Israel. Tukio hili lilifanyika mbele ya Skuli ya Marekani ya Ghaza (American School in Ghaza), ambayo jengo lake zima lilibomolewa na kuharibiwa na mabomu ya Israel miezi sita iliopita. Lengo la mkusanyiko wa wahudumia misaada ya kiutu Ghaza lilikuwa ni kuangaza athari za vikwazo vya Israel dhidi ya sekta ya ilimu na dhidi ya maisha ya watoto wadogo. Philippe Lazzarini, Kaimu Mratibu wa Misaada ya Kiutu kwa Maeneo ya WaFalastina Yaliokaliwa alipohutubia mkusanyiko wa watumishi hawo wa kimataifa aliwaambia vikwazo vya jumla vya Israel dhidi ya Ghaza vimesababisha mateso na maumivu makubwa miongoni mwa watoto, ambao kwa sasa wanakaribia kuanza muda wa masomo, wakati wamezungukwa na mazingira mabaya ya uharibifu mkubwa uliofanyika miezi sita iliopita kutokana na operesheni za kivita za Israel. Kwa mujibu wa taarifa za UM, skuli 18 ziliopo katika Tarafa ya Ghaza ziliangamizwa kwenye mashambulio ya Israel, wakati skuli nyengine 280 zilibomolewa na kuharibiwa vibaya kabisa. Lazzarini alisisitiza ya kuwa mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu Ghaza ni lazima yapatiwe fursa ilio huru, na isiofungwa, kwa wao kuweza kuingia na kutoka kwenye eneo liliokaliwa la Ghaza kuendeleza shughuli zao bila ya pingamizi; hususan ile fursa ya kusimamia huduma muhimu za kufufua tena miundombinu ya ilimu ilioharibiwa na mashambulio yaliopita, maana hivi sasa, aliongeza kusema, imesalia mwezi mmoja tu kabla ya mwaka mpya wa masomo kuanza. Alikumbusha ya kuwa hakuna hata jengo moja la skuli lilioharibiwa na mashambulio ya vikosi vya Israel, lilioruhusiwa kutengenezwa kwa vikwazo dhidi ya vifaa vya kujengea na vifaa vya kufundishia, ikjumlisha vitabu, karatasi na sare za skuli.

Naibu Mkurugenzi wa UM juu ya Huduma za Dharura, Catherine Bragg Ijumanne asubuhi alijumuisha siku ya pili, ya ziara ya siku tano anayoifanya katika Jamhuri ya Afrika Kati (JAK). Siku ya leo alitembelea mji wa Kabo uliopo kaskazini-magharibi ambapo alikutana na viongozi wa kienyeji pamoja na raia waliong'olewa makazi, na vile vile kuonana na watumishi wa jumuia za kimataifa waliopo Kabo. Kabla ya kuondoka huko, Bragg aliwaambia wenyeji kwamba alihuzunishwa sana baada ya kusikiliza taarifa za ushahidi waliotoa raia juu ya shida na maisha magumu wanaokabiliwa nayo kila siku kieneo. Bragg alitoa mwito kwa Serikali ya JAK na pia kwa makundi ya wapinzani, kufuatilia utekelezaji wa maafikiano ya amani, na kuchangisha kipamoja zile juhudi za kurudisha utulivu na amani ya eneo la Kabo. Kadhalika aliwataka wahusika wote kujaribu kuondosha hali ya wasiwasi na khofu miongoni mwa wahamiaji raia ili, hatimaye, kuwawezesha raiahawa kurejea makwao bila matatizo.

Msemaji Mshiriki kutoka Ofisi ya Msemaji wa KM leo aliripoti KM ameingiwa wasiwasi juu ya taarifa za vyombo vya habari juu ya kufumka kwa duru nyengine ya fujo na mapigano ya kimadhehebu, mnamo mwisho wa wiki iliopita kwenye sehemu za Nigeria Kaskazini. Kwa mujibu wa taarifa hiyo KM aliwatumia mkono wa taazia jamaa na aila zote za raia waliopoteza maisha na wale waliojeruhiwa kutokana na fujo hizo. Kadhalika KM alishtumu vitendo vilivyosababisha upotezaji maisha ya watu kihorera na uharibifu wa mali, kutokana na mashambulio ya raia wenye misimamo mikali ya kisiasa. Alitumai wale walioendelza vurugu hili watatambuliwa na kufikishwa mahakamani kwa kufuatana na sheria za kitaifa. Vile vile KM aliisihi Serikali ya Nigeria ikijumuika na taasisi za kutekeleza sheria nchini na zile za usalama, pamoja na viongozi wa kidini na jamii zinazohasimiana kujitahidi kushirikiana kipamoja kukabiliana na vyanzo vya mapigano ya kidini yanayoibuka nchini mwao mara kwa mara, ili waweze kufikia suluhu ya kudumu, kwa kutumia njia za mazungumzo yenye mafahamiano na, hatimaye, kuimarisha hali ya kuvumiliana kitamaduni.