Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya kimataifa yameandaa mradi wa kutoa hadhari za mapema dhidi ya miripuko ya moto

Mashirika ya kimataifa yameandaa mradi wa kutoa hadhari za mapema dhidi ya miripuko ya moto

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) likijumuika na Shirika la Ulaya juu ya Anga Nje ya Dunia (ESA), pamoja na Shirika la Marekani Linalosimamia Uchunguzi wa Anga (NASA) yameripoti juu ya umuhimu wa kudhibiti haraka miripuko ya moto ilioshuhudiwa kutukia ulimwenguni katika siku za karibuni, kwenye sehemu mbalimbali za dunia, hasa yale maeneo ya karibu na Bahari ya Mediterranean, kusini ya Jangwa la Sahara, Australia na katika Amerika ya Kaskazini.

Kwenye taarifa iliotolewa mwanzo wa wiki, UM ulikumbusha ya kuwa udhibiti wa miripuko ya moto kimataifa ni kadhia muhimu kwa afya ya wanadamu, hifadhi ya mazingira na katika usimamizi wa mali ya asili kimataifa. Mashirika matatu ya FAO, ESA na NASA yametangaza kuwa yatatumia vyombo vya setilaiti kusimamia na kufuatilia miripuko ya moto katika dunia, na yataanzisha mpango wa kutahadharisha mapema mataifa juu ya tukio hilo, kwa kuzipatia nchi wanachama takwimu naramani zitakazowaonyesha mahali moto ulipo, na kukadiria aina ya uhai anuwai na viumbe vilivyoangamizwa na moto.