Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa UM ameyakaribisha mazungumzo ya Kamati ya JSC juu ya usalama Usomali

Mjumbe wa UM ameyakaribisha mazungumzo ya Kamati ya JSC juu ya usalama Usomali

Imetangazwa hii leo kwamba Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould-Abdallah, amekaribisha ule mkusanyiko wa wajumbe wa ile Kamati ya Pamoja juu ya Usalama (JSC) uliotukia kwenye mji wa Mogadishu Ijumamosi, mnamo tarehe 25 Julai (2009).

Alisema kikao hicho kiliwasilisha hatua muhimu katika kuleta marekibisho na maendeleo ya udhibiti bora wa usalama nchini Usomali. Alisema Kamati ya Pamoja ya Usalama huipatia Serikali ya Usomali na jumuiya ya kimataifa jukwaa la kushauriana juu ya taratibu za kipamoja, zinazotakikana kuisaidia sekta ya usalama kudhamini shughuli zake nchini, hasa katika kipindi muhimu cha sasa ambapo usalama unaregarega. Kamati ya Pamoja ya Usalama ilibuniwa kwa kulingana na mapendekezo ya Mapatano ya Djbouti kwa madhumuni ya kujadilia masuala ya usalama, ambayo hadidu za rejea za Kamati zimekusudiwa kukabiliana na hali ya usalama ilivyo kwa sasa hivi katika nchi.