Hapa na pale
Catherine Bragg, Naibu Mkurugenzi wa UM Kuhusu Huduma za Dharura na KM Msaidizi wa Misaada ya Kiutu ameanza ziara rasmi ya siku tano katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (JAK). Ijumatatu alizuru Birao, kaskazini-mashariki ya JAK. Wakati atakapokuwepo JAK, Bragg anatarajiwa kufanya tathmini ya hali ya kiutu ilivyo nchini na kuhakikisha misaada ya kihali itahudumiwa, kwa mfululizo, lile fungu la umma muhitaji wenye kutegemea misaada ya kimataifa kunusuru maisha. Bragg analizuru eneo la Birao sasa hivi mwezi mmoja tu baada ya kuripuka mapigano ya kikabila, ambapo watu waliyanganywa mali, nyumba 600 ziliunguzwa moto na raia 3,700 walilazimika kuhajiri makazi kwa sababu ya vurugu.
Ijumatatu Baraza la Usalama lilifanya majadiliano ya hadhara kuhusu suala la Mashariki ya Kati. Oscar Fernandez-Taranco, KM Msaidizi juu ya Masuala ya Kisiasa, alipolihutubia Baraza alieleza kwamba Ofisi yao inasikitika kwamba shughuli haramu za walowezi bado zinaendelea katika Eneo la WaFalastina la Magharibi ya Mto Jordan, liliokaliwa na Israel. Vile vile alisema hali katika Jerusalem Mashariki ni ya kutia wahka mno, kwa sababu ya ujenzi haramu wa majumba unaoongozwa na walowezi wa Israel, wakati majumba ya WaFalastina yakizidi kubomolewa! Kwa upande mwengine, aliongeza kusema, Israel imechukua hatua chache za kutia moyo kidogo pale ilipoamua kupunguza vikwazo dhidi ya haki ya WaFalastina kutembea baina ya miji ya Nablus, Qalqilya, Ramallah na Jericho iliopo Eneo la Magharibi ya Mto Jordan. Kuhusu hali ya kifedha kwenye maeneo yanayotawaliwa na Wafalastina Wenye Madaraka, Fernandez-Taranco alibainisha kuwa hali ni mbaya sana na inahitajia misaada ya dharura. Aliyaomba Mataifa Wanachama, ambayo mnamo siku za karibuni yaliahidi kuchangisha msaada wa kuwahudumia kihali WaFalstina kutekeleza ahadi zao. Juu ya Tarafa ya Ghaza, alisema shida zilizopamba katika eneo hili ni lazima zishughulikiwe haraka na jumuiya kimataifa maana zikiachiwa kuzorotoa kama ilivyo sasa, hakuna atakayefaidika na hali hiyo ya wasiwasi. Fernandez-Taranco alikumbusha pia ya kwamba vifaa vya ujenzi haviruhusiwi na Israel bado kuingia Ghaza, na wakati huo huo bidhaa za Ghaza zimepigwa marufuku kusafirishwa nje ya eneo, hali ambayo alisisitiza "isiokubalika abadan" kimataifa.
Robert Serry, Mratibu Maalumu wa Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati naye kwa upande wake amebainisha kuuingiwa wasiwasi juu ya mizungu inayopitika kwenye eneo la Jerusalem Mashariki ambapo, Ijumapili, walowezi jirani waliteka nyara nyumba ya Mfalastina kwenye ujirani wa Sheikh Jarrah, kufuatia amri ya Mahakama Kuu ya Israel ya kumfukuza nyumbani mwake MFalastina huyo. Kwa mujibu wa Serry, kuongezeka kwa amri za kubomoa nyumba za WaFalastina katika Jerusalem Mashariki na kuwafukuza WaFalastina hawo kutoka kwenye makazi yao ni vitendo vyenye kuharimisha ile Ramani ya Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati. Aliongeza kwa kukumbusha kwamba vitendo vyote vinavyoshadidiwa na walowezi katika eneo liliokaliwa kimabavu la Jerusalem Mashariki, ni vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria ya kimataifa na haviruhusiwi kutumiwa kama ndio hukumu ya kabla hata ya kesi kusikilizwa.
Baraza la Usalama limepokea ripoti ya KM kuhusu maendeleo kwenye utekelzaji wa azimio 1820 juu ya suala la kutumia mabavu ya dhidi ya wanawake. Ndani ya ripoti KM alielezea mchango wake, wa kutumia hadhi ya ofisi yake kutetea vitendo vya kutumia mabavu dhidi ya wanawake vikomeshwe, halan, kampeni ambayo hujumuishwa pia na mradi wa kimataifa unaojulikana kama kampeni ya "UNiTE - Tuungane kukomesha matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake". Kadhalika ripoti ilielezea namna huduma za mashirika ya UM zilivyofungamanishwa kuzuia na kukabiliana na janga ovu hili la kudhalilisha wanawake. Ripoti ilitilia mkazo ya kuwa UM ni lazima uongoze, kwa vitendo, kwenye kadhia hii kwa kuhaklikisha idadi ya wanawake wanaoshiriki katika huduma za kulinda amani za UM ulimwenguni inaongezwa, hasa wanajeshi na polisi. Ripoti ya KM ilisisitiza ya kuwa atahakikisha Naibu KM na maofisa wa vyeo vya juu katika UM watachukua dhamana ziada, za pamoja, za kutetea haki za wanawake kwa lengo la kukomesha matumizi ya mabavu na nguvu yote dhidi ya wanawake, hasa kwenye maeneo ya mizozo na mvutano na baada ya mapigano kusimamishwa.