Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msomi wa Kenya, Ngugi wa Thiong'o, ajumuisha maoni binafsi juu ya 'wajibu wa kimataifa kulinda pamoja raia'

Msomi wa Kenya, Ngugi wa Thiong'o, ajumuisha maoni binafsi juu ya 'wajibu wa kimataifa kulinda pamoja raia'

Alkhamisi asubuhi, kwenye kikao cha Baraza Kuu, kisio rasmi, walikusanyika wataalamu wa kimataifa walioshiriki kwenye majadiliano yenye hamasa kuu, kuzingatia ile rai ya miaka ya nyuma ya kukomesha kile kilichotafsiriwa na wajumbe wa UM kama ni "kiharusi cha kimataifa" katika kukabili maovu na ukatili unaofanyiwa raia, ndani ya taifa, wakati wenye mamlaka wanaposhindwa kuwapatia raia hawa ulinzi na hifadhi wanayostahiki.

Azimio la Wazo la kuwasilisha ‘Wajibu wa Kulinda Raia' lilipitishwa mwezi Septemba 2005 kwenye Mkutano wa Kimataifa, ambapo zaidi ya viongozi 170 wenye kuwakilisha Taifa na serikali, walikubaliana ya kuwa wanawajibika kuimarisha maisha bora, kwa siku za baadaye, kwa lia mwanadamu, kote ulimwenguni. Waliafikiana kwamba ni dhamana ya kila Taifa kuhami na kuwalinda raia dhidi ya mauaji ya halaiki, na kuwakinga na madhara ya makosa ya vita pamoja na kuwahami na jinai dhidi ya utu, na dhidi ya hatari ya vita vya utakaso wa mila za kijadi (ethnic cleansing). Wajumbe wa kimataifa walikubaliana pindi wenye mamlaka ya Kitaifa watashindwa, au hukosa uwezo wa kuwakinga raia dhidi ya jinai hizo, au wakishindwa kuzuia na kukomesha makosa hayo ya kiutu dhidi ya raia zao, jumuiya ya kimataifa itawajibika na kulazimika kuchukua hatua za dharura, kipamoja, kwa ridhaa ya wenye madaraka, kuyasaidia mataifa hayo kuhami raia hawo dhaifu, dhidi ya hatari ya kuangamizwa, kwa kutumia kanuni inayozingatiwa hivi sasa kwenye Baraza Kuu, ijulikanayo kama "wajibu wa kulinda raia" au kwa umaarufu wake huitwa ‘kanuni ya R2P'.

Katika hotuba ya ufunguzi iliotolewa na Raisi wa Baraza Kuu, Miguel d'Escoto Brockmann wa Nicaragua, juu ya uwezekano wa kuidhinisha wazo la kuanzisha ‘kanuni ya R2P', alikumbusha kwamba lengo hasa la sheria hii limekusudiwa kujumuisha ushikamano, miongoni mwa mataifa yote, utakaosaidia kuimarisha haki kwa umma ulio dhaifu, ambao wanajikuta wamenaswa kwenye mazingira yanayohitajia kuukolewa, lakini serikali zao huamua kutochukua hatua zinazofaa kuwanusuru na hali hiyo. Raisi wa Baraza Kuu alisema wajumbe wa kimataifa wanalazimika wajitahidi kuweka kikomo kuhusu majukumu ya aina gani Mataifa yanamudu kuyatekelza kwa raia zao. Alikumbusha kwamba Mataifa yanawajibika kuzuzia mizozo ya kijamii kufumka nchini mwao, kwa kuhakikisha wanashughulikia vyanzo vya mizozo hiyo, mapema, kabla haijasamabaa na kuanza kudhuhuru raia kwa wingi. Kwa hivyo, Raisi wa Baraza Kuu aliutaka UM kuzingatia kidhati uwezo wake wa kuyasaidia mataifa wanachama kuzuia, haraka, vitendo vya jinai ya halaiki visiibuke kwenye yale mataifa yenye kuonyesha dalili za kuambukizwa na hatari hiyo.

Kwenye majadiliano hayo, kama tulivyosema hapo kabla, walijumuika wataalamu mbalimbali kusailia mada anayoizungumzia Raisi wa Baraza Kuu. Miongoni mwa wataalamu waliohudhuria majadiliano haya juu ya wajibu wa kimataifa kulinda raia, au ‘kanuni ya R2P' alikuwemo msomi na mwandishi mashuhuri wa riwaya kutoka Kenya, Profesa Ngugi wa Thiong'o, ambaye hivi sasa anafundisha kwenye Chuo Kikuu cha California cha Irvine, Marekani. Mtayarishaji vipindi wa Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya UM, AZR, alipata fursa ya kufanya mahojiano mafupi na Profesa Ngugi, baada ya kushiriki kwenye majadiliano ya Baraza Kuu juu ya suala hili la ‘wajibu wa kuhami raia'. Alianza mahojiano kwa kumwomba Profesa Ngugi atupatie maoni ya jumla, kuhusu hii rai ya kubuni sheria mpya ya kulinda raia dhidi ya makosa ya jinai ya halaiki, pindi wenye madaraka wanashindwa kuwapatia raia ulinzi unaoridhisha:

NWT: "Ni vizuri kukiwa na uwezo wa kulinda raia, ikiwa serekali imeshindwa, maana tuseme ni wajibu ya kila serekali kulinda watu, na ikiwa serekali haiwezi kulinda watu haina haki ya kutawala. Lakini ni muhimu kuangalia mizizi ya, tuseme mapigano kati ya watu. Ni vizuri kuangalia hali ya uchumi nchini, maana katika Afrika, na nchi nyingi sana, kuna tofauti nyingi sana katika wale walio na mali na wale wasio na mali. Kuna tofauti kubwa sana kati ya mataifa yalio na mali na mataifa walio, tuseme, maskini. Na ukiangalia vizuri rasilmali ya wale wasio na mali ndio inatumiwa wale walio na mali.

AR: Wanatumia kama kisingizio cha kuingilia kati nchi za watu?

NWT: Tuseme hivi, ukiangalia Amerika na tuseme West, Amerika na West, in general, ndio wanatumia rasilmali ya Afrika na Asia na pahali pengine. Lakini wanalipa kitu kidogo tu. Kwa hivyo, utajiri wao ni masikini wetu. Katika kila nchi, tuseme kama Kenya au Amerika kuna mwingine wa wale ambao wana mali ndani ya nchi na maskini - walio na wasio ma mali. Kwa hivyo, kuna tofauti nyingi za mali na .. baina ya mataifa lakini kuna mwengine ndani ya kila taifa na hata ndani ya taifa kuna ... mwingine ambao - sehemu moja ya nchi inaweza kuwa ndio iliendelea mbele sana, na pahali pengine pameachwa nyuma. Kwa hivyo, hiyo tofauti inakuwa mizizi ya kuleta fitina, watu kukasirika na watu kuonea wengine. Kwa hivyo, mimi ninaona vizuri ni kama kungekuwa na mpango wa kumaliza umaskini nchini na umaskini katika mataifa.

AR: Lakini ikiwa sasa hatuko katika kiwango ambacho tunaweza kuzima umaskini wa kimataifa, haya majadiliano namna yalivyoendelea hapa UM, nani atopewa dhamana ya kuamua ni taifa gani ndio linafaa [kuingiliwa na vikosi vya kimataifa] kwa sababu serekali haikufaulu kuwalinda ... raia?

NWT: Yale masuala ni muhimu, na lazima yajadiliwe, na mataifa wote na watu wote, maana hata kuwapatia, tuseme mataifa yaliotajirika, yalio na power uwezo wa kuingilia mataifa ambayo haina nguvu, lakini ... kwa hivyo mimi ninapendelea sana kuongeza nguvu UM, na kufanya UM na idara zake ziwe more democratic, more representative ya watu wote na mataifa yote.

AR: Utawajibu nini wale [wadadisi] ambao wanadai kuwa tunavyo vyombo vya sheria ya kimataifa tayari, kutumiwa kulinda raia. Kwa nini kwa wakati huu tunahitajika chombo kingine kipya cha sheria ya kimataifa?

NWT: Mimi ninapendelea sana kuzingatia, au kuongeza nguvu kwenye yale yaliomo [kwenye sheria ya kimataifa kwa] wakati huu. Hofu yangu ni kusiwe na chombo kingine ambacho kiko outside .. nje ya UM. Nataka kila kitu kiwe ndani, kifanyiwe ndani ya UM. Tena in the long term, ningependa kuona Security Council ikiwa more democratic. Afrika haina sauti katika Security Council na ndio continent pekee, na Australia ambayo haina sauti katika Security Council.

AR: Kwa hivyo, marekibisho ya aina gani ungelipenda kuona yanafanyika katika Baraza la Usalama kuhakikisha ya kuwa ulinzi wa raia unahishimiwa na kila mtu, taifa kubwa na taifa dogo pamoja?

NWT: Taifa kubwa na taifa ndogo wakihishimiana... lakini historia imetuonyesha kwamba mataifa makubwa wakipenda kuinglia mataifa ambayo ni madogo wanaingilia - (AR: hata kama kuna sheria za kimataifa ambazo zinazuia wao kuingilia..) - you know wanaingilia tu. Kwa hivyo, ni muhimu mataifa madogo kuunga mkono vyombo vya dunia au vyombo vya Umoja wa Dunia [Umoja wa Mataifa]. Angalia, kwa mfano, ukiangalia GA, Baraza Kuu, sauti ya mataifa madogo ni kubwa kushinda ilivyo katika Security Council au Baraza la Usalama. Kwa hivyo, ningependekeza mataifa madogo kuunga mkongo vyomba vya UM."

AWK: Huyo alikuwa NWT akichanganua ile mada inayohusu haki ya raia kupatiwa ulinzi wa kimataifa, pindi serikali zao huwanyima hifadhi hiyo kitaifa, dhidi ya ukatili wa halaiki unaopamba ndani ya nchi.

Nikiripoti kutoka Makao Makuu ni AWK wa Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya UM, NY.