Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Kamati ya UM ya Kuondosha Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) ambayo inakutana wiki hii kwenye Makao Makuu ya UM mjini New York, imeanza shughuli za kusailia namna nchi wanachama zinavyotekeleza mikataba ya kimataifa ya kukomesha ubaguzi wa kijinsiya. Kamati hii ya CEDAW imetimia miaka 30 katika mwaka huu. Mwenyekiti wa Kamati ya Kuondosha Ubaguzi Dhidi ya Wanawake, Naela Mohammed Gabr wa kutoka Misri, Ijumatano aliwaambia waandishi habari wa Makao Makuu kwamba miongoni mwa masuala muhimu wanayoyazingatia kwenye kikao cha safari hii ni pamoja na ile mada inayohusu taathira za mizozo ya fedha iliopamba duniani karibuni na namna inavyochafua huduma za kimsingi za jamii. Vile vile alisema Kamati inasailia mada zinazohusu mishahara wanaopatiwa wanawake kwenye mazingira ya mizozo ya kifedha kimataifa, pamoja na tatizo la kuzidi kwa ukosefu wa kazi miongoni mwa wanawake." Kwa mujibu wa taarifa za UM Kamati ya CEDAW hutumia taratibu mbalimbali za kuhamasisha nchi wanachama kutekeleza mapendekezo yake ya kukomesha ubaguzi wa kijinsiya, mathakan, Kamati mara nyingi huchapisha rasmi ukiukaji wa haki za wanawake katika taifa fulani, fafanuzi ambazo baadaye huutumiwa Ofisi ya Kamisheni wa UM juu ya Haki za Binadamu iliopo Geneva. Ofisi ya haki za Binadamu hujumuisha matokeo ya uchunguzi wa Kamati ya CEDAW kwenye ule Mradi wa Mapitio ya Jumla kuhusu namna haki za binadamau zinavyotekelezwa katika Mataifa Wanachama 192 wa UM. Mapitio haya hufanyiwa kila taifa, mara moja katika kila miaka minne. Kwenye mkutano wa wiki hii wataalamu 22 wa Kamati ya CEDAW wanafanyia mapitio juu ya hali za wanawake katika mataifa ya Azerbaijan, Bhutan, Denmark, Guinea-Bissau, Laos, Ujapani, Liberia na pia Uspeni, Uswiss, Timor-Leste na Tuvalu.

Ofisi ya Msemaji wa KM imetangaza kwamba Ban Ki-moon leo amewasili Bejing, Uchina. Ijumaa KM anatazamiwa kufanya mazungumzo maalumu na Raisi Hu Jintao, Waziri Mkuu Wen Jiabao na Waziri wa Mambo ya Kigeni Yang Jiechi, wakijumlisha baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa Uchina atakaokutana nawo kusailia mada mbalimbali muhimu, hususan ile mada inayohusu udhibiti wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Kadhalika mnamo Ijumaa KM atahutubia mkusanyiko maalumu uliokusudiwa kuhimiza raia kutumia balbu za taa zenye kuhifadhi nishati, na ambazo huchukua muda mrefu kumalizika. Anaamini uvumbuzi wa aina hii ya balbu za taa umewasilisha mapinduzi makubwa yenye kuashiria uwezo unaotakikana katika kipindi cha sasa kuimarisha zile juhudi za kudhibiti bora kimataifa athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

KM ametangaza kwamba atafuatilia, kwa ukaribu zaidi, duru ya pili ya uchaguzi ujao wa uraisi katika Guinea-Bissau. Alisema uchaguzi huu ni muhimu sana katika hatua za kuchukuliwa kitaifa kuimarisha mifumo ya kidemokrasia nchini na katika kuleta upatanishi unaoridhisha. KM aliuhimiza umma wa Guinea-Bissau kujishirikisha kwa njia za amani wanapopiga kura, kama walivyofanya kwenye chaguzi zilizopita. Vile vile alitoa mwito maalumu kwa wagombea uraisi unaowataka wajitahidi kama wawezavyo, kusuluhisha mabishano yatakayozuka baadaye kwa kupitia njia za kisheria, na kuwataka pia wahishimu matokeo ya mwisho ya uchaguzi.

Edward Luck, Mshauri Maalumu wa KM, Alkhamisi alihutubia kikao kisio rasmi cha Baraza Kuu, kuzingatia suala la "Wajibu wa Kimataifa Kulinda Raia". Alisema kwenye taarifa yake, binafsi, ya kuwa maadili ya lile wazo linalohusu dhamana ya serikali ya taifa kuwapatia raia hifadhi na ulinzi unaofaa - dhidi ya jinai ya mauaji ya halaiki, na dhidi ya makosa ya vita, pamoja na uhalifu dhidi ya utu, maangamizi ya kimila na utakaso wa makabila - ni wazo linalohishimiwa na mataifa yote ya dunia, hasa ilivyokuwa anaamini, yeye binafsi, kila taifa la ulimwengu limewahi kuteswa na vitendo vya ukatili dhidi ya umma, katika kipindi cha historia yao. Alisema wakashifishaji wa wazo la haki ya jamii ya kimataifa kulinda raia, hulifananisha na kauli ya siri ya kuingilia kati mamlaka ya taifa huru kwa kutumia nguvu za kijeshi ili kuimarisha masilahi ya nchi zenye nguvu. Lakini Luck alisema hakubaliani na mtazamo huu kwa sababu ‘haki ya kulinda raia', anaamini dhamira yake hasa ni kujaribu kuzuia ile tabia ya kikale ya taifa kujiamulia pekee, kuchukua hatua za upande mmoja na ujasiri wa uvamizi wa kijeshi usiolingana katu na kanuni za kimataifa. Alisema zile fikra zinazodai hakuna ulinganifu kati ya dhamana ya kulinda raia na mamlaka huru ya taifa husika ni wazo lisio msingi ambalo analikataa.