Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Utafiti mpya wa Shirika la Afya Duniani (WHO) umegundua ya kuwa mama wajawazito, walioambukizwa na virusi vya UKIMWI wakipewa mchanganyiko wa madawa ya kurefusha maisha, kuanzia kile kipindi cha mwisho wa mimba hadi miezi sita ya kipindi cha kunyonyeshwa mtoto mchanga, asilimia 40 ya watoto wanaozaliwa na mama hawo hunusurika na hatari ya kuambukizwa na virusi vya maradhi. Jumuiya Mashirika ya UM dhidiya UKIMWI (UNAIDS) imeeleza na kukumbusha ya kwamba moja ya malengo muhimu ya kazi zao ni kuhakikisha wanafanikiwa kuzuia vifo vya mama wajawazito, na pia kuhakikisha watoto wachanga wanaozaliwa na mama hawo wanahifadhiwa na maambukizi ya VVU.

KM Ban Ki-moon asubuhi alikutana, faragha, kwenye Makao Makuu ya UM, na Waziri Mkuu wa Iraq, Nouri Kemal al-Maliki. Kwa mujibu wa msemaji wa KM mazungumzo yao yalilenga juu ya utaratibu wa kufanya mapitio ya kifungu cha 5 cha azimio la Baraza la Usalama 1859 (2008), liliozingatia juhudi za kuisaidia Iraq kurudisha hadhi ya kimamlaka, kama ilivyokuwepo kabla ya kupitishwa azimio 661 (1990), chini ya Mlango wa VII ambapo serikali ya Iraq kwa wakati huo ilitafsiriwa na jumuiya ya kimataifa kuhatarisha usalama na amani ya kimataifa pamoja na kuhatarisha utulivu wa nchi jirani. Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Mkuu al-Maliki nchi yake hivi sasa haihatarishi tena usalama au amani, si ya eneo wala ile ya kimataifa. Kwa hivyo aliisihi jumuiya ya kimataifa pamoja na KM kuhakikisha vile vikwazo vilivyowekwa 1990 kudhibiti mamlaka ya Iraq, kwa sababu ya uvamizi wa Iraq dhidi ya Kuwait, kuwa vinafutwa na,hatimaye, kuiwezesha Serikali kudhibiti vyema uhuru wa mamlaka.

Asubuhi KM aliwasilisha mbele ya Baraza la Usalama ripoti yenye kuzingatia ujenzi wa amani wa kitaifa, mara tu baada ya kusitishwa uhasama kwenye eneo la mzozo. Ripoti ilizingatia mwelekeo mpya wa kurudisha amani ambao UM utauratibu na kuusimamia mapema, na kuhakikisha unapatiwa misaada maridhawa ya kukidhia mahitaji hayo. KM alitahadharisha ujenzi wa amani haumaanishi kusimamisha mapigano tu, bali pia humaanisha kuwa na uwezo wa kuanzisha upya taasisi za kizalendo zinazohitajika kuongoza shughuli za utawala, na kurudisha hali ya kuaminiana miongoni mwa raia waliopitia mazingira ya vurugu, itakayowasaidia kuwasukuma kwenye mkondo wa amani ya kudumu kwa siku za baadaye. Ripoti ilizingatia zaidi kile kipindi muhimu cha miaka miwili baada ya uhasama kusimamishwa, ambapo imeonekana hali ya usalama huwa inaregarega kwenye mazingira yanayopambwa na amani dhaifu kabisa.

Kamati ya UM juu ya Utekelezaji wa Haki Zisofutika za Umma wa Falastina Ijumatano imeanza kikao rasmi cha siku mbili, mjini Geneva, kuzingatia suala la Falastina. Kwenye ujumbe aliotuma KM kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa juu ya Falastina, aliisihi Israel kukomesha shughuli zote za kujenga makazi mapya na kupanua majengo ziada kwenye yale maeneo yaliokaliwa ya WaFalastina. Taarifa ya KM ilisisitiza ya kwamba pindi Israel itaendeleea na shughuli hizo, sio itakwenda kinyume na sheria za kimataifa tu bali vile vile itaharimisha maafikiano ya nguvu ya kimataifa dhidi ya hatua hiyo. Kadhalika, risala ya KM ilibainisha kuwa na masikitiko kwa kuwa kundi la WaFalastina la Hamas bado limeshindwa kutangaza kuwa litaachisha matumizi ya nguvu na kuahidi kujihusisha kidhati kutekeleza suluhu ya kuwakilisha Mataifa mawili jirani ya Falastina na Israel, yenye kluishi kipamoja kwa amani.

Dmitri Titov, KM Msaidizi juu ya Taasisi za Usalama na Ufuataji Sheria, kwenye Idara ya UM Inayoshughulikia Operesheni za Ulinzi Amani (DPKO) wiki hii anazuru Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) kusailia mifumo halisi ya majela nchini. Titov aliripotiwa kuzuru eneo la Sake yalipo viwanja vya UM vinavyohudumia shughuli za kufyeka mabomu yaliotegwa kwenye ardhi. Alipokuwepo huko alikutana na maofisa wenyeji wanaoshughulikia masuala ya sheria katika Kivu Kaskazini. Katika mwanzo wa wiki Titov alikuwepo katika Goma na Rutshuru ambapo alizuru jela za huko, na pia alikutana na watumishi raia na wanajeshi wa Shirika la UM Juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC). Kabla ya kuondoka nchini mwisho wa wiki, Titov anatarajiwa kufanya mazungumzo na Mawaziri wa Sheria, Uhusiano wa Kimataifa, Ulinzi na Mambo ya Ndani wa JKK. Titov alianza ziara yake nchini Ijumapili iliopita kwenye mji wa Bunia. Ijumaa inayofuatia Titov atafanya mahojiano na waandishi habari katika JKK juu ya matokeo ya ziara yake.