Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ashraf Qazi, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Sudan na Mkuu wa Shirika la Ulinzi Amani Sudan Kusini (UNMIS) ameripotiwa hii leo kuelekea eneo la mgogoro wa mpaka la Abyei, kwenye mkesha wa kutangazwa na Mahakama ya Upatanishi wa Abyei kutoka Hague maamuzi kuhusu eneo la mfarakano baina ya Sudan Kaskazini na Kusini. Uamuzi utatolewa na Mahakama ya Upatanishi Ijumatano. Mjumbe wa KM kwa Sudan Kusini alinakiliwa akisema hatua zimeshachukuliwa na wenye madaraka, za kuhakikisha makundi yote yenye silaha, isipokuwa Vikosi vya Pamoja vya Polisi na Jeshi, yameondoshwa kutoka Eneo la Mfarakano la Ramani ya Abyei kabla ya maamuzi kutangazwa kuzuia fujo.

Asubuhi, KM Ban Ki-moon aliwakilisha ripoti maalumu mbele ya Baraza Kuu la UM juu ya mada inayohusu ‘Wajibu wa Kulinda Raia'. Alisema kwenye risala yake kwamba wakati umewadia kwa jamii ya kimataifa kutekeleza, kwa vitendo halisi, zile ahadi zilizotolewa 2005 za kudhaminia kihakika ulinzi wa raia kwenye mamlaka ya utawala pakikosekana hifadhi ya wenye madaraka. Aliongeza kusema ya kuwa hivi sasa tumejaaliwa fursa ya kutumia "uwezo wa mkusanyiko wa kimataifa na nia imara ya pamoja, kukabiliana na matishio yaliofanana na ule ukatili uliojiri miaka ya nyuma katika Rwanda". Alikumbusha, utaratibu uliojumuishwa kwenye ripoti yake unafungamana na nguzo tatu kuhusu maadili ya kimataifa: dhamana ya taifa kuhami na kulinda raia waliomo kwenye utawala huru; msaada wa kimataifa na ujenzi wa uwezo unaotakikana kudhibiti bora ulinzi wa raia; na kuhudumia itiko la dharura, kwa wakati, bila ya mashaka, inapohitajika." Ripoti ya KM ilisisitiza kwamba dhamana ya kulinda raia wanaonyimwa ulinzi na wenye mamlaka ni jukumu linalotakiwa kusimamiwa na UM, chini la tabaka la maadili ya Mkataba wa UM. KM alitoa mwito kwa Mataifa Wanachama kuliruhusu Baraza Kuu kuandaa jukwaa la kuongoza majadiliano ya kuleta maafikiano yatakayoridhisha pande zote husika na yatakayoweza kutekelezwa bila matatizo juu ya suala la nani mwenye ‘haki, dhamana na jukumu la kulinda raia wanaoteswa kitaifa.' Lengo la majadiliano haya ni kufuatilia maafikiano yaliopitishwa na viongozi wa kimataifa mnamo 2005 ya kuwapatia raia kinga dhidi ya "mauaji ya halaiki na makosa makuu mengine yanayokiuka haki za binadamu yanayoendelezwa kwenye mataifa yao, hali ambayo itailazimisha jumuiya ya kimataifa kuingilia kati pale wenye madaraka wanaposhindwa kuwapatia raia ulinzi unaofaa kunusuru maisha."

Taarifa iliotolewa na msemaji wa KM, baada ya mahojiano ya Ijumanne adhuhuri na waandishi habari wa kimataifa, ilishtumu kwa kauli kali yale matukio ya Ijumatatu ya katika miji miwili ya Usomali, ambapo ofisi za UM zilihujumiwa na kuibiwa vifaa na makundi ya upinzani. Vitendo hivi, ilisema taarifa ya KM, vilikusudiwa kutia dosari operesheni zote za UM zinazosimamia misaada ya kiutu na ulinzi wa amani katika Usomali. Hata hivyo, taarifa ilisisitiza, UM umeshaahidi kuwa utaendelea kuupatia umma muhitaji wa Usomali misaada ya kunusuru maisha na kuliwezesha taifa hilo kujifufua kutoka yale mazingira ya vurugu yalioselelea nchini kwa miongo kadha ili, hatimaye, kuruhusu mazingira ya usalama na amani kurejea kieneo.

Ripoti juu ya Maendeleo ya Kiutu katika Nchi za KiArabu kwa 2009 iliotolewa Ijumanne na Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) imeeleza usalama uliouponyoka umma wa nchi za KiArabu ndio chanzo kinachodhoofisha huduma za maendeleo kwa ujumla kwenye ukanda wao. Ilisema ripoti mara nyingi usalama wa umma katika eneo hili hutishwa na mifumo ya kiuchumi, jamii na kisaiasa isio ya haki; hali ambayo pia huchochewa na mashindano ya kuwania nguvu ya madaraka na uchotaji wa rasilmali miongoni mwa makundi yaliogawanyika vipande vipande; na mara nyengine, ripoti iliongeza kusema, usalama wa umma pia huathirika kutokana na uvamizi wa majeshi ya kigeni kwenye maeneo ya nchi za KiArabu.

Ijumanne asubuhi Baraza la Usalama lilikutana kwenye kikao makhsusi kuzingatia masuala ya usalama na amani katika bara la Afrika. Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa, B. LynnPascoe aliwahutubia wajumbe wa Baraza kuhusu maendeleo ya karibuni kwenye mvutano wa kisiasa baina ya mataifa jirani ya Eritrea na Djibouti.