Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO kuhadharisha Bonde la Mto Zambezi lasibiwa maradhi yanayouwa samaki

FAO kuhadharisha Bonde la Mto Zambezi lasibiwa maradhi yanayouwa samaki

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limehadharisha kwenye ripoti yake rasmi iliotolewa Ijumanne, ya kwamba kumegundulikana aina ya maradhi yenye kuua na kupunguza kwa kiwango kikubwa akiba ya samaki kwenye Bonde la Mto Zambezi, hali ambayo inahatarisha akiba ya chakula na ajira ya kujipatia rizki kwa wakazi wa vijijini wa eneo hilo, liliogawanyika miongoni mwa mataifa saba ya Afrika.

Taifa liliaothriika zaidi na masaibu haya ni Zambia ambapo ilipo thuluthi mbili ya bonde la Mto Zambezi. Taarifa ya FAO ilieleza aina ya kuvu waliopo kwenye Mto Zambezi, husababisha vidonda vibaya kwenye ngozi ya samaki na kuleta vifo vya haraka kwa fungu kubwa la samaki. Rohana Subasinghe, Ofisa Mkuu wa FAO anayeshughulikia Rasilmali ya Samaki alitoa onyo linalosisitiza ya kuwa "bila ya tatizo hili kudhibitiwa haraka na wataalamu wa kimataifa, kuna hatari kuu ya maradhi haya kusambaa kwenye mataifa mengine jirani yanayolizunguka Bonde la Mto Zambezi, na vile vile kuathiri mito kijumla, kwenye eneo hilo."