Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raisi mstaafu wa Ghana ameteuliwa na WFP kusaidia kukomesha njaa inayosumbua watoto

Raisi mstaafu wa Ghana ameteuliwa na WFP kusaidia kukomesha njaa inayosumbua watoto

Raisi mstaafu wa Ghana, John Kufuor, ameteuliwa rasmi na Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) kuwa Balozi Mtetezi mpya dhidi ya Njaa Duniani.

Anatarajiwa kushiriki kwenye kampeni za kuihamasisha jumuiya ya kimataifa, kuchangisha misaada maridhawa ya kuhudumia lishe bora kwa watoto milioni 66 katika ulimwengu, watoto ambao huwa wanahudhuria skuli kila siku pasipo kupata chakula. Kufuor alisema "lengo muhimu la maadili ya kimataifa, kwa sasa hivi, ni kuona kila kiongozi wa dunia huwa anahakikisha kila mtoto ulimwenguni hupatiwa lishe bora"; lengo ambalo alisema atalihudumia kikamilifu na kuona linatekelezwa kwenye mataifa yote ya dunia. Ilivyokuwa idadi ya umma wenye njaa inatarajiwa kufikia bilioni moja katika mwaka huu, Josette Sheeran, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la WFP alisisitiza, kwenye taarifa yake kwamba uteuzi wa Raisi mstaafu wa Ghana kuwa Balozi Mtetezi dhidi ya njaa utasaidia pakubwa kuuhudumia umma huo. Kama Balozi wa WFP, Kufuor anatarajiwa kutilia mkazo kwenye shughuli zake juu ya umuhimu wa uwekezaji wa muda mrefu kwenye maendeleo ya kilimo, na katika kuhamasisha wahisani wa kimataifa kuongeza mchango wa kulisaidia Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) kuhudumia vyema misaada ya chakula kwa umma muhitaji wa kimataifa.