Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICRC inazingatia udhibiti wa biashara haramu ya silaha ndogo ndogo ulimwenguni

ICRC inazingatia udhibiti wa biashara haramu ya silaha ndogo ndogo ulimwenguni

Kwa muda wa angalau miaka kumi hivi, Kamati ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (ICRC) ilijishirikisha kwenye jitihadi za kuyashawishi Mataifa Wanachama wa UM, kwa ujumla, kubuni kanuni kali mpya zitakazotumiwa kudhibiti biashara haramu ya silaha ndogo ndogo duniani.

Hivi sasa, Mkuu wa Kitengo Kinachohusika na Masuala ya Silaha katika Idara ya Sheria ya Kamati ya ICRC, Peter Herby, anashirki kwenye majadiliano na UM juu ya uwezekano wa kuanzisha vikao vya kimataifa ili kusailia suala hili. Mtayarishaji wa vipindi vya Kiingereza katika Redio ya UM, Diane Bailey, alipata fursa ya kumhoji mwakilishi huyo wa ICRC, ambaye alianza kwa kueleza sababu zilizoifanya taasisi yao kujihusisha na suala la kuwepo mkataba wa kudhibiti silaha ndogo ndogo duniani, hasa baada ya yeye binafsi kushuhudia madhara maututi, kwa raia, yanayotokana na biashara haramu ya silaha hizi:

"Taathira ya silaha ndogo ndogo, na hasa fursa ya watu kuwa na uwezo wa kuzipata silaha hizo kwa urahisi, ni jambo ambalo kwenye shughuli zetu za kazi, tunalishuhudia kila siku. Hapa ninamaanisha kwamba biashara haramu ya silaha ndogo ndogo ndio inayowafanya wafuasi wa yale makundi ya mgambo, yenye silaha, kuwashikia bunduki watoto wadogo, chini ya umri wa kisheria, na kuwalazimisha kujiunga nao kwenye fujo, vurugu na mapigano haramu. Kimsingi, ninaweza kusema miongoni mwa mambo yanayoshuhudiwa na watu wenye kuzuru hospitali zetu, pamoja na zahanati za tiba katika sehemu kadha wa kadha za dunia, ni madhara yanayoletwa kwa raia na kusababishwa na matumizi ya silaha ndogo ndogo."

Vile vile Ofisa huyu wa Kamati ya ICRC alieleza kwamba kwa sababu ya ukosefu wa sheria ya kimataifa inayotambuliwa na nchi wanachama, kuongoza na kusimamia biashara ya silaha nyepesi na silaha ndogo ndogo, wachuuzi wa biasahara hii ndio hujipatia fursa haramu ya kueneza biasahara yao katika shemu mbalimbali za ulimwengu, hususan kwenye lile soko huru la kimataifa linalosimamia biashara ya magendo ya silaha. Alisema watu wingi hufaidika na biashara hii haramu. Lakini anaamini pindi jumuiya ya kimataifa itawania na kushirikiana kwa nguvu moja, kubuni mkataba mpya ulio imara, na unaoridhisha, kudhibiti biashara ya silaha hizo, natija kubwa zitapatikana kwenye juhudi za kusaidia kutunza maisha ya mamilioni ya umma wa kimataifa wanaodhurika na tatizo la silaha ndogo ndogo. Alikumbusha ya kuwa mifano ya kuhalalisha pendekezo hilo upo tayari pale jumuiya ya kimataifa iliposhirikiana kubuni kanuni za sheria ya kimataifa kudhibiti biashara ya kemikali hatari kwa wanadamu na pia sheria za kudhibiti biashara ya madawa kwenye soko la kimataifa.

Kwa hivyo kwa kufuatana na misingi ya kimantiki, Peter Herby alisema Mataifa Wanachama yanawajibika kubuni sheria kali ya kimataifa, itakayotumiwa kudhibiti bora biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na silaha nyepesi ambazo hudhuru wanadamu na kusababisha maafa aina kwa aina kimaisha. Kwenye mahojiano na Redio ya UM, Peter Herby alitupatia maoni yake, kama ifuatavyo, akielezea kwa nini hatua hiyo imezorota, na Mataifa Wanachama yameshindwa kuitekeleza kama inavyotakikana:

 "Bila shaka kuna upinzani mkubwa usiopendelea biashara ya silaha ndogo ndogo kudhibitiwa na taasisi za kimataifa, kwa sababu wadau hawa wa biashara ya silaha ndogo ndogo huifananisha huduma hii na furushi kubwa la fedha zenye kuwatajirisha, kadhia ambayo vile vile huathiri sera za kitaifa na kimataifa; na kwa upande mwengine, yale mataifa yanayohusika na biashara hii huamini umilikaji wa shughuli hizo ni muhimu kwa usalama wao. Kwa hivyo, tukipendekeza kuzingatiwe suala hili la biashara ya silaha ndogo ndogo na nchi wanachama, huona tumezingiwa na tunajikuta kutonesha hisia za usalama wa taifa husika, kwa kulingana hasa na wale wenye kufaidika na biashara hiyo. Lakini mara nyingi fungu hili la Mataifa, na washirika wao, huwa wanasahau kwamba lengo la kuanzisha majadiliano ya kubuni mkataba mpya wa kudhibiti silaha ndogo ndogo haimaanishi silaha hizo zitapokonywa wale waliozipata kwa njia za halali, ikijumlisha pia Serikali za Mataifa. ... Mkataba wa kudhibiti biashara ya silaha ndogo ndogo, kusema kweli, umekusudiwa hasa kuhakikisha upatikanaji wa silaha hizo utakuwa unaoongozwa kwa kanuni za kimataifa zinazotambulikana rasmi na Mataifa Wanachama, huduma ambayo itarahisisha utekelezaji hakika wa maadili ya UM katika kuimarisha haki za binadamu, kuendeleza amani, usalama, utulivu na pia kuongeza nguvu ya kuhishimu sheria."