Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon ameshtumu, kwa kauli kali, mashambulio ya mabomu yaliofanyika leo Ijumaa kwenye hoteli mbili za Jakarta (Indonesia), ambapo taarifa ya kwanza inasema watu tisa waliuawa. Taarifa ya KM kuhusu tukio hili ilielezea juu ya ushikamano wake na Serikali pamoja na umma wa Indonesia, na alisisitza kwamba anatambua juhudi thabiti za Serikali ya Indonesia katika kukabiliana na matatizo ya ugaidi, kwa ujumla. Alisema anatumai Serikali ya Indonesia itafanikiwa kuwafikisha mahakamani wale waliohusika na mashambulio hayo. KM aliwatumia mkono wa taazia aila zote za waathiriwa wa mashambulio na pia kuwaombea majeruhi wapone haraka.

Ripoti ya KM kuhusu operesheni za Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID), iliotolewa rasmi Ijumaa, ina maelezo kuhusu matatizo kadha yaliovikabili vikosi hivyo tangu vilipoanza kuenezwa kwenye jimbo la magharibi la Sudan, kuanzia miezi 18 iliopita. Ripoti ilipongeza ushirikiano mzuri uliopo sasa hivi kati ya taasisi ya UNAMID na Serikali ya Sudan. Kadhalika, KM aliashiria asilimia 92 ya vikosi vilivyoahidiwa na Mataifa Wanachama kupelekwa Darfur vitakamilishwa kuenezwa huko katika tarehe 31 Disemba 2009. Vile vile ripoti ilieleza hali za raia, kwa ujumla, katika Darfur bado ni za wasiwasi - watu milioni 2.6 walisajiliwa kung'olewa makazi na hawawezi tena kurejeshwa makwao kwa sasa; WaDarfuri milioni 4.7 wanahitajia kuhudumiwa misaada ya kihali kumudu maisha ya kawaida, na wakati huo huo ujambazi na vitendo vya kunajisi kimabavu wanawake vinaendelea kuwasumbua raia.

Heraldo Munoz, Mwenyekiti wa Tume ya UM Inayochunguza Kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Benazir Bhutto, Ijumaa aliwaambia waandishi habari katika mji wa Islamabad, Pakistan Ijumaa kwamba timu yake inaahidi itatekeleza majukumu yake kwa uwazi unaoridhisha, na ipo tayari kupokea ushauri unaofaa, na pia imejishurutisha kuhakikisha ukweli wa mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu, utatambulika kihakika na kufahamika. Kabla ya hapo Balozi Munoz na timu yake walizuru Rawalpindi, kwenye lile eneo ambalo Benazir Bhutto aliuawa.

Mjumbe Maalumu wa KM juu ya Amani ya Cote d'Ivoire, Choi Young-Jin ametoa mwito unaohimiza kuchapishwa, haraka, jedwali mpya ya utaratibu wa kufanyisha uchaguzi wa taifa. Alikhofia pindi mradi wa uchaguzi hautotekelezwa kama ilivyoafikiwa na makundi husika nchini, na kuruhusu raia kupiga kura katika tarehe 29 Novemba 2009, kuna hatari ya uchaguzi huo wa uraisi kucheleweshwa zaidi.

Mnamo alasiri ya Ijumamosi ya tarehe 18 Julai 2009, KM Ban Ki-moon atahudhuria tamasha maalumu kuadhimisha kufikia miaka 91 kwa aliyekuwa Raisi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, taadhima itakayofanyika kwenye Steshini Kuu ya Reli ya Grand Central kwenye jiji la New York. Miongoni mwa mapendekezo yaliohusikana na taadhima hizi ni ile rai ya Raisi Mandela iliohimiza kila mtu, kujitolea, angalau dakika 67, kuhudumia umma muhitaji wa kimataifa. Watu walihimizwa kujiandikisha kwenye ile Hati ya Msokoto ya Majina ya Watu Wanaojitolea ambayo itaenezwa katika sehemu kadha wa kadha za kimataifa. KM aliahidi atajitolea dakika 67 za kazi kuhudumia umma, kwa hishima ya Nelson Mandela ambaye KM alisema ni kiongozi "anayejumuisha maadili kamili, ya thamani ya juu kabisa ya UM."