Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC imekabidhiwa ushahidi ziada juu ya fujo kufuatia uchaguzi uliopita Kenya

ICC imekabidhiwa ushahidi ziada juu ya fujo kufuatia uchaguzi uliopita Kenya

Luis Moreno-Ocampo, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Halaiki (ICC) ameripotiwa kupokea wiki hii taarifa ziada kuhusu vurugu na fujo zilizozuka Kenya baada ya uchaguzi uliopita.

Ocampo alikabidhiwa ripoti mbili kutoka Mwanasheria Mkuu wa Kenya, na katika siku zijazo atapokea ripoti ziada za ushahidi wa uthibitisho kutoka Kofi Annan, Mwenyekiti wa Tume Maalumu ya UA ya Watu Mashuhuri, ripoti zilizohifadhiwa ndani ya maboksi sita, ushahidi uliokusanywa na Kamisheni ya Uchunguzi wa Vurugu la Baada ya Uchaguzi Kenya - Kamisheni inayojulikana kwa umaarufu kama Kamisheni/Tume ya WAKI. Kadhalika, Tume ya WAKI hii ilituma barua yenye orodha ya majina ya watuhumiwa waliohusika na fujo za baada ya uchaguzi nchini Kenya. Kwa mujibu wa Mahakama ya ICC, yaliyomo ndani ya barua hiyo yatabaki kuwa faragha, na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka itatumia taarifa zote walizopokea kuendeleza utafiti kabla ya kuamua kama kutahitajika kufanyika uchunguzi ziada kufungua kesi au la.