Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Bei za chakula kwenye nchi maskini bado ni za juu sana' kuhadharisha FAO

'Bei za chakula kwenye nchi maskini bado ni za juu sana' kuhadharisha FAO

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limewasilisha ripoti mpya yenye kuhadharisha ya kuwa bei za chakula za ndani ya nchi, kwenye mataifa kadha yanayoendelea, zimesalia kuwa za juu sana, licha ya kuwa kimataifa bei za chakula, kijumla, zimeteremka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha karibuni, ambapo pia palishuhudiwa mavuno mazuri ya nafaka.

Mada ya ripoti imepewa jina linalosema Hali ya Chakula na Matarajio ya Baadaye ya Mazao. Ripoti ilibainisha kwamba katika baadhi ya nchi, bei za vyakula zilikiuka viwango vya mwaka uliopita, hali ambayo imesababisha shida nyingi za kimaisha kwa mamilioni ya watu ambao tangu mwanzo wamebanwa na hali duni. Kwenye mataifa ya Afrika, kusini ya Jangwa la Sahara, asilimia 80 mpaka 90 za bei zote za nafaka katika zile nchi 21 zilizofanyiwa uchunguzi na FAO, zimeonekana kubakia kuwa ni za juu, kwa kima cha asilimia 25, kuzidi bei za chakula zilizokuwepo miaka miwili nyuma, kabla ya mzozo wa chakula kufumka na kuenea kimataifa. Kwa mujibu wa ripoti, bei ya mtama, mwezi Juni, kwenye maeneo ya Afrika Mashariki na Sudan, ilizidi kwa mara tatu ile bei ya miaka miwili iliopita. Kadhalika, bei ya mahindi katika mataifa ya Uganda, Kenya na Ethiopia imegundulikana kuongezeka maradufu, tukilinganisha na bei ya miaka miwili nyuma. Lakini katika eneo la Kusini mwa Afrika, bei ya mahindi huko inaripotiwa kuteremka kwa sababu ya mazao mengi mno yaliovunwa kwenye miezi ya karibuni; na hata hivyo bei ya chakula Kusini mwa Afrika bado imesalia kwa kima kilichozidi bei iliopo katika kipindi kabla ya mzozo wa chakula kujiri kimataifa. Miongoni mwa masuala yaliodhihirishwa kuchochea bei za juu za chakula kuselelea katika nchi masikini, inajumuisha kupungua kwa mavuno kieneo, kuchelewa kwa bidhaa za chakula kuingia nchini kutoka nchi za kigeni, na pia kupamba kwa mizozo ya wenyewe kwa wenyewe nchini, na vile vile kuongezeka kwa mahitaji ya chakula katika mataifa jirani, pamoja na mfuatano wa biashara ya kigeugeu ya kikanda, na pia kuteremka kwa thamani ya fedha za kitaifa, ikichanganyika na mabadiliko katika sera za kibiashara na sera za chakula pamoja na gharama kubwa za usafirishaji wa chakula.