Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Wajumbe watatu wa Tume ya Uchunguzi wa kutafuta ukweli, na kusailia mazingira yaliosababisha mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Benazir Bhutto wanatazamiwa kuwasili Pakistan mnamo siku za karibuni kuenedelza shughuli zao. Tume hii ilianzisha kazi zake rasmi tarehe 01 Julai (2009), na ziara yao Pakistan itakuwa ya awali nchini humo. Madaraka yailiodhaminiwa Tume na Baraza la Usalama, baada ya kushauriana na Serikali ya Pakistan, ni kuchunguza ukweli wa mauaji ya Benazir Bhutto na sio kufanya upelelezi wa uhalifu unaohusikana na kitendo hicho. Jukumu la upelelezi wa uhalifu na kuendesha mashitaka kwa wakosaji ni dhamana ya wenye mamlaka Pakistan. Ripoti ya matokeo ya uchunguzi wa Tume inatarajiwa kukabidhiwa KM katika miezi sita ijayo - mnamo mwisho wa Disemba 2009.

Naibu KM juu ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM Duniani, Alain Le Roy Ijumanne alizuru El Geneina, Darfur Magharibi, karibu na mipaka na Chad. Alipokuwepo huko alikutana na Wali (Gavana) wa jimbo na kusailia naye mada kadha zinazohusu usalama, uenezaji haramu wa silaha na masuala mengine yanayoambatana na amani ya eneo. Wakati El Geneina Le Roy alipata pia fursa ya kukutana na baadhi ya wale wahamiaji wa ndani 2,100 waliorejea Darfur Magharibi, kwa khiyari, mnamo siku za karibuni baada ya utulivu kurudishwa vijijini, umma ambao Le Roy aliushuhudia ukishiriki kwenye shughuli kadha za kilimo. Kadhalika Le Roy alikutana na viongozi wengine wa kijadi kwenye eneo, pamoja na wawakilishi wa wazee wa eneo, wanawake na vijana na kusikiliza maombi yao. Le Roy anatarajiwa kurejea New York mwisho wa wiki na Ijumaa atalipatia Baraza la Usalama fafanuzi halisi juu ya hali katika Sudan.

Charles Taylor, aliyekuwa Raisi wa Liberia, leo alipata fursa ya kujitetea binafsi mbele ya Mahakama Maalumu juu ya Vita katika Sierra Leone, iliopo kwenye mji wa Hague, Uholanzi. Mahakama ilimshtaki Taylor kuhusika na makosa ya vita na jinai dhidi ya utu mnamo miaka iliopita katika Sierra Leone. Taylor alikana mashtaka yote 11 dhidi yake, ikijumlisha makosa ya kushiriki kwenye ugaidi, makosa ya kuua, vitendo vya kutesa watu na udhalilishaji wa kijinsiya. Alisema Taylor tuhumu na madai ya mwendesha mashtaka dhidi yake yalikuwa ya kupotosha, yaliojaa udanganyifu na alisisitiza madai hayo yaliambatana na tetesi zisio msingi wala ukweli. Kadhalika Taylor alikana kuwa aliwasaidia wafuasi wa kundi la waasi la Sierra Leone la RUF (Revolutionary United Front) kupalilia uhasama nchini. Mawakili watetezi wanatazamiwa kuendeleza utetezi wao mnamo wiki sita zijazo na hukumu ya kesi inatarajiwa kutolewa mwaka ujao.

Mashirika yanayohudumia misaada ya kihali yametoa mwito wa kutaka yafadhiliwe msaada wa dola milioni 11 kusimamia miradi ya dharura ya ugawaji wa maji safi na usafi wa mazingira, kwa ule umma unaojumuisha watu 600,000 waliong'olewa makazi kwa sababu ya mapigano yalioshtadi Mogadishu katika wiki za karibuni, uhasama ambao umeselelea kieneo tangu 2007. Kaw mujibu wa Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA), mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu sasa hivi yanamudu kutoa msaada wa maji safi ya lita 2 mpaka 8, kila siku, kwa kila mtu mmoja kwenye eneo wanamoishi wahamiaji wa ndani walionyimwa mastakimu ya kawaida. Taarifa za afya zinasema kikawaida mwanadamu huhitajia, kwa wastani, baina ya lita 7.5 mapaka 15 za maji kuweza kunusuru maisha. Ukosefu wa maji safi, iliripoti OCHA, ndio tatizo lenye kuathiri sana zile juhudi za kimataifa za kudhibiti na kuzuia kuenea kwa maradhi ya kuambukiza kwenye maeneo yaliosongomana ya umma uliong'olewa makazi Usomali.