Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwezo wa kufanyiza dawa ya chanjo dhidi ya A(H1N1) ni mdogo, ahadharisha mkuu wa WHO

Uwezo wa kufanyiza dawa ya chanjo dhidi ya A(H1N1) ni mdogo, ahadharisha mkuu wa WHO

Imeripotiwa na UM kwamba uwezo uliopo sasa wa kutengeneza chanjo kinga dhidi ya homa ya mafua ya aina ya A(H1N1) ni mdogo na hautoweza kukidhi mahitaji ya watu bilioni 6.8 waliopo ulimwenguni sasa hivi, idadi ambayo inakabiliwa na uwezo wa kuambukizwa kirahisi na kuathirika na virusi vipya hatari vya homa hiyo.

Bayana hii ilitolewa na Dktr Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) alipohutubia Geneva mkutano wa Shirika la UM juu Ya Hakimiliki za Taaluma Duniani (WIPO). Alikumbusha hali ilivyo sasa inaelekea akiba kubwa ya chanjo ya kupambana na homa ya mafua ya A(H1N1) itafaidisha zaidi nchi tajiri badala ya mataifa muhitaji maskini, hali yenye kuonyesha dhahiri hata katika mazingira ya maradhi yenye kuhatarisha ulimwengu mzima watakaofaidika zaid na tiba dhidi ya maradhi hayo ni nchi zenye uwezo wa kulipa. Lakini Dktr Chan pia alisema kwenye hitilafu za huduma za tiba baina ya nchi masikini na matajiri, wataalamu pia hupata fursa ya kuhamasishwa kuzalisha dawa mbadala zenye uwezo wa kuyasaidia mataifa maskini kukidhi mahitaji ya tiba ya homa ya mafua kwa umma wao. Chanjo bora inayofikiriwa na wataalamu wa afya dhidi ya homa ya mafua ni ile yenye uwezo wa kuuhami umma dhidi ya virusi vya homa ya majira na dhidi ya ile homa yenye kuenea kila mahali. Aliwahimiza wataalamu kuharakisha tafiti zao ili kusaidia kuvumbua chanjo hiyo mpya kwa masilhai ya umma mzima wa kimataifa.