Mashirika ya UM kuanzisha Kituo cha Isange kuhudumia waathirika wa mabavu Rwanda
Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Wanawake (UNIFEM) limeripoti kutiwa sahihi maafikiano ya pamoja, kati ya mashirika ya UM na Serikali ya Rwanda, ya kuanzisha kituo maalumu cha kuwahudumia kihali na kiakili wale wanawake na watoto wanaoteswa na vitendo vya kutumia nguvu na mabavu dhidi yao.
Taasisi hii itajulikana kama Kituo cha Isange. Isange kwa lugha ya Kinyarwanda humaanisha "makaribisho huru yenye mapokezi yasio vizingiti" kwa wateswa wa vitendo vya kutumiliwa nguvu na mabavu, ambao huhitaji matibabu, na msaada wa kisheria pamoja na tiba ya kiakili, ikichanganyika na huduma za kijamii, kwenye mazingira yanayoridhisha na yenye kuaminika. Katika utafiti wa karibuni uliondelezwa bia baina ya UNIFEM na Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda, kusailia matatizo ya kujamiana kimabavu na makosa ya kijinsia, waathirika na walionusuruika na karaha hiyo waliripoti kwamba mazingira yanayotishia katika mahospitali, polisi na mahakama huwanyima fursa za kuripoti makosa hayo bila khofu. Huduma za kukabiliana na makosa kama hayo zipo, ilidhihirisha matokeo ya utafiti, lakini "zimetawanyika na huwanyima waathirika uwezo wa kutoa ushahidi kwa wenye madaraka badala ya kuwasaidia kurahisisha huduma hiyo." Kituo cha Isange kinatazamiwa kuwekwa kwenye Hospitali ya Polisi ya Kacyriu iliopo Kigali, na kitawapatia waathirika huduma kadha wa kadha, ikijumlisha hifadhi dhidi ya kuteswa tena, fursa ya kufanyiwa upelelezi wa makosa ya jinai, uangalizi wa matibabu na kupatiwa taarifa za kuwakilishwa mahakamani, na vile vile kupata tiba ya "kimwili na matibabu ya kukomesha kihoro cha kiakili kinachowavaa waathirika wa mateso husika." Huduma hizi zitakamilishwa kwa sababu ya ushirikiano baina ya huduma za Afya ya Polisi wa Kitaifa Rwanda na mashirika yaliopo nchini ya UM ikijumlisha shirika la mfuko wa maendeleo kwa wanawake, UNIFEM; mfuko wa kudhibiti idadi ya watu, UNFPA na mfuko wa maendeleo kwa watoto, UNICEF.