Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ad Melkert, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Iraq ameripoti kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulio ya karibuni nchini, ambapo Wakristo walio wachache walihujumiwa pamoja na taasisi zao za kidini na makundi yasiotambulikana. Alieleza hisia hizo baada ya makanisa kadha kushambuliwa Ijumapili katika miji ya Baghdad na Mosul, mashambulio yaliosababisha vifo vya watu wanne na darzeni za majeruhi. Melkert alisema "kampeni hii ya vurugu imekusudiwa kupalilia vitisho miongoni mwa makundi yalio dhaifu, na kwa lengo la kuzuia watu wa dini tofauti kuishi pamoja kwa amani, kwenye moja ya eneo maarufu miongoni mwa chimbuko kuu la kimataifa lenye kujumlisha anuwai za kidini na kikabila. Melkert alitoa mwito uyatakayo makundi husika yote, ikijumlisha Serikali ya Iraq, kuongeza mara mbili zaidi jitihadi zao za kuwapatia wazalendo walio wachache ndani ya nchi, hifadhi kinga na kuimarisha anuwai ya kidini, kikabila na kitamaduni iliopo katika Iraq kwa karne kadha wa kadha.

Ijumapili Choi Young-Jin, Mwakilishi Maalumu wa KM kwa Cote d'Ivoire alikutana na Raisi Laurent Gbagbo, ikiwa miongoni mwa mikutano anayofanya kikawaida na makundi ya kizalendo, ambapo hupata fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu maandalizi ya uchaguzi ujao wa taifa. Mwakilishi wa KM alisema alithibitisha pia ya kuwa usajili na utambulisho wa raia wanaostahiki kupiga kura ulishakamilishwa nchini mnamo tarehe 30 Juni (2009), na anabashiria mwelekeo wa kutia moyo kwamba raia wapo tayari kuyatekeleza majukumu waliodhaminiwa ya kusimamia uchaguzi kama inavyotakikana kisheria. Alisema kilichosalia kwa sasa ni kuzingatia utaratibu utakaohakikisha kutakuwepo juhudi za pamoja kudhibiti mbinu halisi za kiufundi zitakazotumiwa kuendesha uchaguzi utakaofanyika rasmi tarehe 29 Novemba 29 (2009), tarehe ambayo alitumai itahishimiwa na makundi yote husika.

Naibu Katibu Mkuu juu ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM Duniani, Alain Le Roy, akifuatana na Kamishna wa Usalama na Amani wa Umoja wa Afrika, Ramtane Lamamra, Ijumatatu walianza ziara ya pamoja ya siku mbili katika Darfur. Walikutana na Wali (Gavana) Othman Kabir wa Darfur Kaskazini na kujadiliana naye hali ya eneo kijumla, ikijumuisha masuala ya kiutu, wahamiaji na mradi wa uchaguzi. Kadhalika, ujumbe wa Le Roy na Lamamra ulikutana na viongozi wa kijadi (Umdas), na wale wanaowakilisha vijana na wanawake waliotokea Abu Shouk, na kufanya mazungumzo vile vile na wahamiaji wa ndani wa kambi ya Al Salaam. Le Roy aliwaambia Shirika la Mchanganyiko la UM-UA kwa Darfur la UNAMID, litaendelea na shughuli za kuhakikisha mahitaji yao yanatekelezwa, na raia husika huwa wanapatiwa hifadhi wanayostahiki, kwa ushirikiano na mashirika yasio ya kiserikali; na kuongeza kwamba mashirika ya kimataifa yatajitahidi kuharakisha kukamilisha idadi ya vikosi vya mchanganyiko vay UM-UA vinavyohitajika kuendeleza utulivu na amani katika Darfur.

Ripoti iliotolewa bia na Jumuiya ya Mashirika ya UM Dhidi ya UKIMWI (UNAIDS) na Waqf wa Aila ya Kaiser imebainisha ahadi ya mchango wa misaada ya fedha kutoka nchi zilizoendelea katika 2008 - ikjumlisha zile nchi wanachama wa Kundi la G-8, Kamisheni ya Ulaya na serikali wafadhili nyenginezo - zilifika dola bilioni 8.7, muongezeko wa kuridhisha tukilinganisha na jumla ya mwaka mmoja kabla ya hapo, ambapo kulichangishwa dola bilioni 6.6. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baina ya miaka 2002 na 2008, ahadi ya kuchangisha msaada wa fedha wa kukabiliana na VVU na UKIMWI, na ugawaji wa misaada hiyo kutoka mataifa yalioendelea uliongezeka kwa mara tano. Lakini ripoti vile vile ilikumbusha mchango huo ulifanyika kabla ya miripuko ya mizozo ya kiuchumi iliotanda duniani kwa sasa hivi, mizozo ambayo ina hatari ya kuzusha matatizo kadha wa kadha ziada kuhusu ukusanyaji mpya wa misaada kutoka wafadhili wa kimataifa kukabili UKIMWI.