Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Siku ya Udhibiti wa Idadi ya Watu Duniani itaadhimishwa rasmi mwaka huu na UM mnamo Ijumamosi ya tarehe 11 Julai 2009; na mada ya safari hii inasema "Tuwekeze mchango wa maendeleo kwa masilahi ya wanawake na watoto wa kike." UM unaamini uwekezaji miongoni mwa watoto wa kike na wanawake, utakaowapatia fursa ya kipato utawafanya kuwa raia wenye uwezo na madaraka ya kuzalisha matunda yatakayochangisha pakubwa kwenye zile juhudi za kitaifa katika kufufua na kukuza uchumi wa kizalendo. Kadhalika utasaidia kuwapatia watoto wao wa kike ilimu yenye natija kimaendeleo, na kuwapa taarifa kinga juu ya afya bora, uzazi wa mpangilio na madaraka ya uhuru wa kujiamulia kimaisha.

KM Ban Ki-moon Ijumatatu asubuhi anatazamiwa kuripoti kwenye Baraza la Usalama kuhusu ziara yake ya wiki iliopita katika Myanmar. Ijumaa ya leo KM alimalizia ziara ya wiki mbili alioifanya katika mataifa ya Asia na Ulaya kwenye mji wa L'Aquila, Utaliana ambapo alikuwa amehudhuria Mkutano Mkuu wa mwaka wa nchi wanachama wa Kundi la G-8. Kabla ya kuondoka L'Aquila kuelekea New York mnamo siku ya leo, KM alikuwa na majadiliano na viongozi wa G-8 kuhusu amana ya chakula ulimwenguni. Alitahadharisha kwenye risala yake ya kuwa idadi ya watu wenye njaa sugu, inayoendelea kukithiri ulimwenguni, hivi sasa imekiuka watu bilioni moja - kiwango ambacho alisisitiza KM hakijawahi kushuhudiwa kihistoria. Alipendekeza kuanzishwe miradi ya jumla ya kilimo, ya muda mfupi na muda mrefu, itakayohudumiwa, kwa kupitia taasisi za kikanda, kukuza juhudi za kizalendo za mataifa maskini.

Ripoti mpya ya KM kuhusu Cote d'Ivoire iliowasilishwa leo Ijumaa, imetoa nasaha yenye kuyahimiza makundi ya kisiasa yaliopo nchini, kuhishimu tarehe ya kufanyika uchaguzi iliowekwa rasmi mwezi Mei na wenye mamlaka. Tarehe hiyo ni 29 Novemba (2009). Ripoti vile vile iliyataka makundi husika kuhakikisha uchaguzi utaendeshwa kwa utaratibu ulio huru, wa haki, wenye uwazi na unaoaminika. Alisema KM ndani ya ripoti ya kuwa ana matumaini kutachapishwa, bila ya kuchelewa, kikomo cha muda wa kuyakamilisha yale majukumu yaliosalia ya mpango wa amani kabla ya uchaguzi haujafanyika, hususan lile suala la mungano halisi wa taifa.

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK asubuhi aliwasilisha ripoti yake kuhusu hali ya usalama na shughuli za MONUC katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Doss alisema kwenye taarifa hiyo, hatua zilizochukuliwa kukongoa yale makundi yenye silaha katika JKK mashariki, zimezusha wasiwasi miongoni mwa sekta fulani za kimataifa, hususan namna hatua hizo zinavyoathiri raia. Alisema mashambulio ya kulipiza kisasi yaliofanywa na makundi ya waasi wa FDLR na LRA, dhidi ya raia, vile vile yalisababisha idadi kubwa ya watu kung'olewa makazi na kuendelzwa vitendo vilivyoharamisha haki za binadamu kwa kiwango kilichofurutu ada. Kwa mujibu wa Doss kuna baadhi ya askari wa Jeshi la Taifa la FARDC, wasio nidhamu, ambao pia walinaswa wakiendeleza vitendo haramu dhidi ya raia. Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC), alikumbusha Doss, sasa hivi linashughulikia miradi kadha wa kadha muhimu ya kulinda raia dhidi ya mashambulio ya waasi, ikijumlisha pia kadhia ya kueneza vikosi vya MONUC kwenye majimbo ya mashariki yenye matatizo. Kadhalika, alikumbusha Mjumbe wa KM, MONUC imejishirikisha kikamilifu kuhudumia raia na kuwapatia hifadhi bora dhidi ya vitendo haramu vya kutumia mabavu na udhalilishaji wa kijinsia.

Wakandarasi wa ujenzi wanaotumikia UM wameripotiwa kuwa wameanzisha shughuli za kusafisha vifusi viliyozagaa kwenye eneo liliokaliwa la WaFalastina la Tarafa ya Ghaza kufuatia yale mashambulio ya operesheni za vikosi vya Israel, yaliofanyika mwanzo wa mwaka. Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP), ambalo linahusika na huduma ya kusafisha vifusi vya majengo yaliobomolewa Ghaza, uondoshaji wa tani 420,000 za vifusi katika eneo ni mwanzo muhimu wa kusaidia umma wa eneo kujipona kiakili na uharibifu ulioletwa na uvamizi dhidi yao. Mradi wa kusafisha vifusi unatazamiwa kutekelezwa kwa mwaka mmoja mfululizo, na ni hatua itakayosaidia kuwapatia ajira wakazi wa Ghaza na pia kuimarishia mazingira yao, kabla hawajaanzisha tena ujenzi wa majumba yaliobomolewa na mashambulio ya vikosi vya Israel.