Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la chakula laikabili Sudan Kusini, inahadharisha UNMIS

Janga la chakula laikabili Sudan Kusini, inahadharisha UNMIS

David Gressly, Mratibu wa misaada ya kiutu kwa Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani Sudan Kusini (UNMIS) ameripoti wiki hii ya kuwa Sudan Kusini inakabiliwa na hatari ya kuzuka janga kuu la chakula, kwa mwaka huu, kwa sababu ya mvua haba ilionyesha katika majimbo kadha, na vile vile kutokana na ukosefu wa usalama, hali ambayo ilisambaratisha sana shughuli za kilimo, katika mazingira ambayo mioundombinu dhaifu iliopo nchini imezorotisha zaidi zile shughuli za mashirika ya kimataifa za kugawa misaada ya kiutu ya kunusuru maisha kwa umma muhitaji wa eneo hilo.

 Kwa mujibu wa UNMIS majimbo yatakayoathirika hasa ni yale ya Bahr-el-Ghazal Kaskazini, Jonglei na Nile ya Juu ambapo huishi watu milioni tatu, kwa kulingana na takwimu rasmi zilizochukuliwa 2008 na Serikali. Kadhalika eneo la Ikweta Mashariki nalo pia linakhofiwa litaathirika na tatizo la chakula. Eneo la Akobo, ambapo watu 19,000 waliong'olewa makazi huishi, limekabiliwa na matatizo magumu ya chakula kufuatia tukio la tarehe 12 Juni ambapo mashua zilizokuwa zimebeba shehena ya chakula zilishambuliwa, karibu na eneo la Nassir, kwenye Jimbo la Nile ya Juu.