Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano ya kikabila Sudan Kusini yawalenga wanawake na watoto wasiohatia

Mapigano ya kikabila Sudan Kusini yawalenga wanawake na watoto wasiohatia

Mapigano ya kikabila, yaliosajiliwa kupamba hivi karibuni katika Sudan Kusini, yalionyesha kulenga mashambulio yake zaidi dhidi ya fungu la umma ambao hauhusikani kamwe na mvutano huo, yaani wanawake na watoto wadogo, kwa mujibu wa taarifa iliotangazwa wiki hii na Joseph Contreras, Naibu Ofisa wa Habari kwa Umma wa Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani Sudan Kusini (UNMIS).

Mapigano haya yaliripotiwa kusababisha vifo vya karibu watu elfu moja. Katika siku za nyuma, uhasama kama huu ulizusha vifo zaidi miongoni mwa vijana wa kiume, waliokuwa wakilinda mashamba ya mifugo ya ng'ombe. Lakini katika wiki za karibuni, mashambulio yameshuhudiwa kuvamia hata raia, kama anavyoeleza hapa Naibu Ofisa wa Habari wa Shirika la UNMIS, Joseph Contreras:

 "Tangu mwanzo wa mwaka, tulishuhudia baadhi ya mapigano ya kikabila yalioliambukiza jimbo la Sudan Kusini yalisababisha idadi kubwa ya vifo na majeruihi miongoni mwa wanawake na watoto wadogo, tukilinganisha na hali ilivyokuwa katika miaka uliopita .. ."

Alisema baadhi ya mashambulio yaliofanyika kieneo kwenye miezi ya karibuni, hasa katika miezi ya Machi na Aprili mwaka huu, katika mikoa ya Akobo na Pibor, kwenye Jimbo la Jonglei (Sudan Kusini) idadi kubwa ya wafu ilijumuisha vijana watoto na wanawake. Aliongeza kusema kwamba wapiganaji sio huwalenga wanawake na watoto wadogo tu, bali huhakikisha pia kundi kundi hili la raia ndilo litakaoathirika zaidi na kujumlisha idadi kubwa ya vifo, licha ya kuwa wanawake na watoto vijana hawahusikani kamwe na mapigano."

Shirika la UNMIS limeripoti kwamba hali kwa ujumla Sudan Kusini kwa sasa ni ya kigeugeu, na wasiwasi wa kimaisha umetanda miongoni mwa makabila yenye kuishi huko, kwa sababu ya kuwepo ushindani mkali wa kugombania umilikaji wa rasilmali ziliokuwepo kwenye eneo miongoni mwa jamii za makabila tofauti. UNMIS sasa hivi imetuma jumla ya wanajeshi na watumishi wa kiraia 120 kwenye Jimbo la Jonglei, kwa makusudio ya kusaidia kurudisha tena hali ya utulivu na amani kwenye eneo la mvutano la Sudan Kusini.