Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM amehadharisha viongozi wa G-8 kwamba uamuzi wao wa kupunguza hewa chafu hauridhishi

KM amehadharisha viongozi wa G-8 kwamba uamuzi wao wa kupunguza hewa chafu hauridhishi

KM Ban Ki-moon Alkhamisi ya leo alihutubia kikao maalumu, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Viongozi wa Mataifa Yenye Uchumi Mkuu wa Kundi la G-8, unaofanyika kwenye mji wa L\'Aquila, Utaliana.

Aliwaambia wawakilishi wa mataifa husika, kwenye hotuba yake, kwamba ahadi walizotoa kwenye risala zao kuhusu udhibiti wa mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni zinakaribishwa, lakini, alisema KM, haziridhishi kwa sababu hazilingani na mapendekezo halisi ya maamuzi ya kisayansi yanayozitaka nchi zenye maendeleo ya viwandani kupunguza, kwa kiwango kikubwa zaidi, umwagaji wao wa hewa chafu kwenye anga. Alisisitiza, Serikali za nchi zenye maendeleo ya viwanda zinahitajika kuongeza mchango wao katika kudhibiti bora athari za mabadiliko ya hali ya hewa, hali ambayo itasaidia kuyakamilisha, kwa mafanikio, maafikiano mapya kwenye kikao kijacho cha Copenhagen kitakachokutana mwezi Disemba mwaka huu. Alisisitiza ya kuwa "wakati hatunao tena wa kuchukua hatua za nusu nusu, au kuchelewesha utekelezaji wa kadhia hiyo." Alitahadharisha ikiwa mataifa yaliowakilishwa kwenye kikao cha L'Aquila yatashindwa kuchukua hatua hakika za kupunguza hewa chafu kwa mwaka huu, yatapoteza fursa ya aina pekee kihistoria. KM alisema maafikiano ya wanachama wa G-8 kupunguza umwagaji wa hewa chafu kwa asilimia 80 itakapofika 2050 ni hatua ya kutia moyo, na aliongeza, kwa kusema maafikiano yao kuweza kuaminika yatahitajia nia kuu itakayotangaza kwayo vigezo hakika vya muda maalumu wa kuyatekeleza mapendekezo ya kupunguza hewa chafu angani.