Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya KM imethibitisha kukithiri ukiukaji wa haki za binadamu katika JKK

Ripoti ya KM imethibitisha kukithiri ukiukaji wa haki za binadamu katika JKK

Ripoti mpya ya KM juu ya shughuli za Shirika la Ulinzi Amani la UM katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (MONUC) imeeleza hali ya amani nchini humo, kwa ujumla, inakabiliwa bado na vizingiti kadha wa kadha.

Mathalan, katika sehemu za mashahriki, ripoti inasema, hali ya usalama huko bado ni ya kigeugeu na ya hatari. Ripoti ilibainisha zile operesheni za kijeshi dhidi ya vikundi vya kigeni vyenye silaha na wale waasi wa kizalendo, zimeyafanya makundi haya haramu kuamua kushambulia raia, badala yake, hali ambayo imewalazimisha raia kuhajiri makazi yao kwa idadi kubwa kabisa kunusuru maisha, tukio ambalo vile vile liliongeza ukiukaji wa haki za binadamu ulioendelezwa na waasi dhidi ya raia. Vitendo haramu hivi vinajumlisha udhalilishaji wa kijinsia na matumizi ya mabavu dhidi ya wanawake, jinai ambayo mara nyengine huendelezwa hata na vikosi vya usalama vya Serikali. Juu ya masuala ya kutumia nguvu na kunajisi wanawake, ripoti ilisema mara nyingi makamanda wa kijeshi, wakichanganyika na maofisa wa polisi wanaoendeleza upelelezi wa matukio kama hayo huonekana wakijaribu kuwashawishi waathirika kukubali suluhu ya makosa haya ya kijinsia, nje ya mahakama, hali ambayo inakhofiwa ndio inayopalilia tabia karaha na ovu ya wakosa kutenda uhalifu bila kuogopa kuadhibiwa.