Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO latangaza umuhimu wa kuwepo mtandao wa kupambana na maradhi yasioambukiza

WHO latangaza umuhimu wa kuwepo mtandao wa kupambana na maradhi yasioambukiza

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kwamba licha ya kuwa maradhi yasioambukiza – kama ugonjwa wa moyo, kiharusi, saratani, kisukari, pamoja na magonjwa ya pumu na yale majeraha ya kikawaida – ndio maradhi yenye kujumlisha idadi kubwa ya vifo ulimwenguni, hata hivyo, wahisani na mashirika ya kimataifa bado wanashindwa kuyapa maradhi haya umuhimu yanayostahiki na kuyafungamanisha na zile sera zinazoambatana na miradi ya kukuza maendeleo.

Wakati Baraza la UM juu ya Maendeleo ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) linakutana wiki hii kwenye mji wa Geneva, Uswiss kuzingatia udhibiti bora wa afya ya jamii kimataifa, viongozi kadha wa kadha wanaoshugulikia afya na maendeleo wanatazamiwa kutoa miito maalumu ya kuihimiza jamii ya kimataifa kufungamanisha viashirio vya maradhi yasioambukiza na majeraha ya kawaida, na zile sera zenye kutathminia utekelezaji wa mafanikio wa viini vya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs).