Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera za uwekezaji kwenye nchi za G-20 zaonyesha kinaa

Sera za uwekezaji kwenye nchi za G-20 zaonyesha kinaa

Ripoti ya mapitio ya Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD), juu ya uwekezaji katika vitega uchumi wa kitaifa na kimataifa, imeeleza uchunguzi wao umebainisha zile nchi wanachama wa kundi la G-20 zimejizuia, kwa sasa, kuchukua hatua za dharura kudhibiti uwekezaji ndani ya nchi na katika mataifa ya nje, licha ya kuwa ulimwengu, kwa ujumla, unakabiliwa na mizozo aina kwa aina ya kiuchumi na kifedha.

Kusema kweli UNCTAD imegundua sera za wanachama wa kundi la G-20 husisitiza na kurahisisha huduma za uwekezaji kwenye maeneo yao. Ripoti hii ya UNCTAD imewakilishwa katika kipindi ambapo uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje umeonekana kuporomoka, takriban katika mataifa mengi duniani, hususan kwenye mataifa yanayoendelea. Lakini mwelekeo wa wanachama wa kundi la G-20 unadhihirisha nchi hizi zimekinai na hali ilivyo kimaendeleo, kwa sababu katika kipindi kilichofanyiwa ukaguzi - yaani baina ya Oktoba 2008 mpaka Juni 2009 - kulibuniwa sheria chache mpya za kiuchumi na mataifa haya, kwa lengo la kudhibiti athari za mizozo ya uchumi katika soko la kimataifa. Hata hivyo, ripoti imeonya dhidi ya hatari ya ile tabia ya mataifa husika, yaani mataifa ya G-20, kujiona yameridhika kiuchumi, kwa sababu ya kufadhiliwa na serikali zao mafurushi maridhawa ya fedha zilizotumiwa kuchochea uchumi wao uliozorota. Mwelekeo huu, ilihadharisha UNCTAD, hutafsiriwa na mataifa yenye uchumi haba kama ni "sera werevu za kulinda viwanda vya kizalendo" vya mataifa ya G-20 dhidi ya waekezaji wa nje.