Skip to main content

Matatizo ya uchumi duniani hozorotisha juhudi za kuzuwia na kutibu VVU katika nchi masikini

Matatizo ya uchumi duniani hozorotisha juhudi za kuzuwia na kutibu VVU katika nchi masikini

Tukiendelea na ripoti nyengine juu ya masuala ya uchumi wa kimataifa, Benki Kuu ya Dunia na Jumuiya Mashirika ya UM dhidi ya UKIMWI (UNAIDS) leo yamewasilisha ripoti ya pamoja, yenye kuthibitisha nchi 22 katika Afrika, na kwenye maeneo ya Karibian, Ulaya na Asia ya Kati pamoja na zile sehemu za Asia na Pasifiki, yatakabiliwa na misukosuko na vizingiti kadha wa kadha kwenye utekelezaji wa majukumu yanayohusu miradi ya kutibu na kuzuia maambukizi ya VVU kwa mwaka huu, kwa sababu ya mizozo ya uchumi iliopamba duniani.

Mada ya ripoti inasema ‘Mzozo wa Uchumi Duniani na Miradi ya Kutibu na Kukinga Maambukizi ya VVU: Madhara na Athari Zake.' Kwa mujibu wa ripoti, kutokana na taarifa zilizokusanywa na watumishi wa mashirika ya UM yaliopo katika nchi 71, zilionyesha nchi nane zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa zile dawa za kurefusha maisha na kusambaratisha huduma nyenginezo za udhibiti bora wa maradhi haya maututi. Nchi hizi hujumlisha asilimia 60 ya yale maeneo yanayofadhiliwa matibabu ya kudhibiti UKIMWI duniani.