Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM ameeleza Ijumatatu, kwenye mazungumzo aliokuwa nayo na waandishi habari Geneva, kwamba alihuzunishwa sana, binafsi, na tukio liliosababisha watu kupoteza maisha wakati wanaandamanaji katika Honduras waliposhiriki kwenye mdhahara wa kumuunga mkono Raisi José Manuel Zelaya Rosales ambaye aliondoshwa madarakani kimabavu na wanajeshi katika wiki za karibuni. KM alisema raia, kokote walipo ulimwenguni, wana haki ya kutoa maoni hadharani na uhuru wa kusema, bila ya kukhofia vitisho wala hujuma za kimabavu kutoka kwa wenye mamlaka. Alisisitiza, mabadiliko yeyote ya utawala, yasiolingana na katiba, hayakubaliki katu na jumuiya ya kimataifa na hayana uhalali katika sheria za kimataifa.

Kadhalika, kwenye mahojiano na waandishi habari wa Geneva KM alizungumzia kuhusu vurugu liliozuka mwisho wa wiki katika Jimbo la Uchina la Xinjiang. Alikumbusha, kwamba kwa kuambatana na tukio hili nchi wanachama zinawajibika kutatua, kwa njia za amani, tofauti ziliopo za kimawazo kati ya raia wanaopingana, na kwa kutumia majadiliano ya ana kwa ana badala ya mapigano. Alisema haiwafalii wenye madaraka kutumia nguvu kusuluhisha hali ya kutofahamiana miongoni mwa raia na serikali. Aliisihi Serikali ya Uchina kutumia hadhari kubwa, na kuchukua hatua zinazofaa, kuhakikisha maisha ya raia huwa yanahifadhiwa, na usalama wao unatunzwa kama unavyostahiki.

Tume iliodhaminiwa na Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu, kuchunguza, na kutafuta ukweli juu ya mashambulizi yaliotukia mwisho wa 2008 na mwanzo wa mwaka huu, dhidi ya eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza, tume inayoongozwa na Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini, leo imeanzisha rasmi duru ya pili ya kusikiliza ushahidi wa hadhara uliotolewa na waathirika, mashahidi na wataalamu wa kutokea Israel kusini na pia kutokea eneo liliokaliwa la Wafalastina la Ufukwe wa Magharibi ya Mto Jordan. Ushahidi ulitolewa na watu binafsi, na kwa wale wasiomudu kwenda Geneva ushahidi wao waliutoa kwa kupitia njia ya vidio. Tume inatarajiwa kutangaza ripoti juu ya uchunguzi wao mwezi Agosti.

Baraza la Usalama limekutana Ijumatatu alasiri kuzingatia uzuiaji wa usambazaji wa silaha za nyuklia kimataifa, kwa kufungamana na ukakamavu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea/Korea ya Kaskazini (DPRK). Kwa mujibu wa taarifa za UM, DPRK iliendeleza majaribio saba ya makombora kwenye mwambao wa taifa, mnamo tarehe 04 Julai 2009, kitendo ambacho wajumbe 15 wa Baraza wanaamini kimeonyesha dharau ya maazimio yake yaliopitishwa hapo kabla ambayo yaliamrisha DPRK kusitisha haraka vitendo hivi. Kuhusu azimio 1874 (2009) liliopitishwa na Baraza la Usalama mwezi uliopita, liliweka hatua kadha za vikwazo dhidi ya DPRK, zilizojumuisha ruhusa ya kukagua meli za DPRK zinazotiliwa shaka kuchukua shehena zilizopigwa marufuku, shehena ambazo hudhaniwa zitatumiwa katika shughuli za kutengeneza makombora na kwenye miradi ya kinyuklia nchini humo. Vile vile azimio lilipendekeza kukaza sheria za kuzuia silaha kuingizwa katika DPRK, isipokuwa zile silaha nyepesi, na pia kuongeza vikwazo vya kifedha dhidi ya DPRK.

Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Halaiki (ICC) leo imeanzisha mfululizo wa vipindi vya redio katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (JAK) vilivyokusudiwa kuwafunza umma juu ya kazi, shughuli na madaraka ya mahakama. Vipindi 13 vinatarajiwa kutangazwa, kwa kutumia lugha ya kienyeji ya Kisango, kwenye steshini za redio 14 tofauti. Mradi huu umefanikiwa kutekelezwa baada ya kufanyika vikao karibu 50 vya ICC, vilivyoendelezwa kati ya miezi ya Januari mpaka Juni 2009, katika mji mkuu wa Bangui, mkusanyiko ambao ulitumiwa kuwafunza umma juu ya shughuli za mahakama. Jamhuri ya Afrika ya Kati ni moja ya maeneo manne katika Afrika - yakijumlisha pia Darfur katika Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) na Uganda - ambayo yanachunguzwa na Mwendesha Mashitaka wa ICC kwa hivi sasa, kuhusika na madai ya makosa ya jinai ya halaiki. Mahakama ya ICC ni mahakama huru ya kudumu, inayoongwa mkono na UM, na imeanzishwa kushughulikia kesi za watu waliotuhumiwa kushiriki kwenye mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya utu na jinai ya vita.