Skip to main content

UNHCR yafadhilia utafiti wa athari za KiIslam kwenye sheria ya hifadhi ya wahamiaji

UNHCR yafadhilia utafiti wa athari za KiIslam kwenye sheria ya hifadhi ya wahamiaji

Profesa Ahmed Abu al-Wafa, mtaalamu wa sheria katika Chuo Kikuu cha Cairo, ameandika kitabu chenye jina lisemalo "Utafiti wa Kulinganisha: Haki ya Kupata Hifadhi na Usalama Baina ya Shari\'ah ya KiIslam na Sheria ya Kimataifa ya Wahamiaji".

Nadharia ya kitabu inajaribu kukumbusha, kwa kuthibitisha ukweli wa kihistoria, juu ya namna mila na tamaduni za KiIslam, zilizokuwa zikitumiwa kwa miaka 1,400 ziada kuhudumia wahamiaji na wakimbizi, kwa ukarimu usio ubaguzi, zilivyojumuishwa kwenye sheria ya kimataifa juu ya hifadhi ya wahamiaji. Kitabu kilichapishwa bia na Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR), Chuo Kikuu cha Kiarabu cha Naif, katika Saudi Arabia pamoja na Umoja wa Nchi za KiIslam (OIC), na kiliwasilishwa rasmi kimataifa katika tarehe 23 Juni (2009). Profesa Abu al-Wafa anaelezea ndani ya kitabu, hoja mbalimbali za kitaaluma, zenye kuthibitisha namna Shari'ah (sheria ya KiIslam) na mila za KiIslam, kwa ujumla, zinavyothamini na kuhishimu haki za wahamiaji na wale wakimbizi wenye kuomba hifadhi, hata ikiwa umma huo ni wafuasi wa dini tofauti. Taarifa ya Shirika la UM juu ya Wahamiaji (UNHCR) iliotolewa kwa waandishi habari juu ya kitabu cha Profesa Abu al-Wafa, ilieleza ya kuwa kwa kulingana na kanuni za dini ya KiIslam, ni haramu na vibaya kwa mtu au taifa, kuwalazimisha wahamiaji wasio WaIslam kubadili dini. Kadhalika, kanuni hizo ziliwakumbusha wafuasi na taasisi zote zinazopokea wahamiaji, kuwa wanawajibika kisharia kutowalazimisha wahamiaji wasio WaIslam kuregeza imani yao au kubadilisha dini. Vile vile maadili ya UIslam yanaamrisha wenyeji wenye kutoa hifadhi wajitahidi, kama wawezavyo, kuhakikisha kuwa aila zilizolazimika kuhama makwao, kutafuta hifadhi kwenye maeneo mengine, kwa sababu ya maafa au vurugu, kuwa aila hizo hazitotengwa, na kuahidi familia hizo zitakutanishwa pamoja kwenye maeneo mapya yenye usalama na utulivu. Kadhalika wenyeji wanatakiwa kuhakikisha maisha na mali za wahamiaji hawa huwa zinadhaminiwa na kutunzwa, kwa ulinzi wa hadhi ya juu kabisa, kama invyostahiki kisharia.

António Guterres, Kamishna Mkuu wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) mnamo siku zanyuma alipendekeza kufanyike utafiti maalumu wa kitaaluma, kusailia na kubainisha kihakika fungamano ziliopo za mila za KiIslam na haki za wahamiaji wenye kuomba hifadhi.

Sikiliza ripoti kamili kwenye idhaa ya mtandao.